Sababu UDSM kuibeba ajenda ya madini wiki ya utafiti
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia utafiti, Profesa Nelson Boniface akizungumzia wiki ya utafiti na ubunifu ya chuoni hapo.
Muktasari:
- Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaibeba ajenda hiyo ikiwakutanisha wadau kwenye sekta ya madini, wanataaluma na wanafunzi.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikielekea kwa kasi katika matumizi ya nishati jadidifu na teknolojia za kidijitali, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeamua kuweka mezani mjadala wa namna utajiri wa madini uliopo Tanzania unavyoweza kuwa nguzo ya maendeleo ya taifa katika karne hii.
Mjadala huo utakuwa sehemu ya Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yatakayofanyika kuanzia Juni 9 hadi 11, 2026 katika Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere, yakibeba kaulimbiu isemayo “Kutumia Utajiri wa Madini Yanayopatikana Nchini Tanzania katika Kukuza Nishati Jadidifu, Mageuzi ya Dijitali na Usalama wa Jamii.”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface, maadhimisho hayo yatafunguliwa Juni 9 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, katika Ukumbi wa Nkrumah, huku yakihitimishwa Juni 11 kwa hafla ya utoaji wa tuzo itakayoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo.
Profesa Boniface amesema kaulimbiu ya mwaka huu imechaguliwa kwa kuzingatia umuhimu wa madini ya kimkakati kama grafiti, nikeli, lithiamu, kobalti na urani katika kuendeleza sekta ya nishati jadidifu, pamoja na mchango wa grafiti, madini adimu ya ardhi (REEs), shaba na dhahabu katika mageuzi ya kidijitali.
Amesema maonesho na mijadala mbalimbali itaonesha jinsi rasilimali hizo zinavyoweza kuchochea ubunifu, kuongeza uwezo wa kiteknolojia na kuharakisha mpito kuelekea uchumi unaotegemea teknolojia na nishati safi.
Mbali na maonesho ya tafiti na ubunifu, washiriki watapata fursa ya kushiriki makongamano, mijadala ya kitaalamu, shughuli za kujenga mtandao wa ushirikiano na majadiliano kuhusu namna ya kugeuza matokeo ya tafiti kuwa bidhaa na huduma zenye manufaa kwa jamii na uchumi.
Rais wa Singapore kuhutubia
Katika hatua nyingine , Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, atatoa muhadhara wa wazi kwa umma Juni 9 katika UDSM akiwa nchini kwa ziara ya kikazi.
Muhadhara huo unatarajiwa kuwakutanisha wanafunzi, watafiti, wasomi na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kujifunza kutokana na uzoefu wa Singapore katika kujenga uchumi unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia.
Aidha, Juni 10 kutafanyika majadiliano maalumu ya ushirikiano wa kimkakati yatakayowakutanisha wawakilishi kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi, viwanda na Serikali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kujadili mbinu za kuongeza thamani ya madini kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Katika kilele cha maadhimisho hayo, UDSM itatambua mchango wa watafiti na wabunifu kupitia tuzo tisa zitakazotolewa kwa makundi mbalimbali, ikiwemo mtafiti bora wa mwaka, mbunifu bora wa mwaka, mradi bora wa utafiti, pamoja na miradi bora ya ubunifu kwa wanafunzi wa shahada za awali na uzamili.
Profesa Boniface amesema jukwaa hilo ni sehemu ya juhudi za UDSM kuendelea kutumia utafiti kama kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku akiwakaribisha wadau wote kushiriki katika mjadala huo unaolenga kuibua fursa mpya za maendeleo kupitia matumizi bora ya rasilimali za madini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ujasiriamali na Ubunifu wa UDSM, Profesa Lilian Kaale amesema chuo hicho kwa sasa kimeweka nguvu kwenye ubunifu na kuhakikisha tafiti na maandiko ya kitaaluma hayaishii kwenye makaratasi.
“Tunataka kuangalia matokeo ya tafiti na bunifu zetu zinamfikia mlaji wa mwisho ndiyo maana tumeweka nguvu kwenye kuwajengea uwezo wanafunzi wetu, ili tafiti na bunifu wanazofanya ziongezewe thamani na kuleta tija kwenye jamii,” amesema.