Sababu zinazochangia wanaume kuongoza magonjwa afya ya akili

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya ya akili na wanasaikolojia wametaja sababu 10 zinazochangia wanaume kuongoza kuugua magonjwa ya afya ya akili ikilinganishwa na wanawake.

  

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya ya akili na wanasaikolojia wametaja sababu 10 zinazochangia wanaume kuongoza kuugua magonjwa ya afya ya akili ikilinganishwa na wanawake.

Sababu hizo ni kuzongwa na majukumu, ugumu wa maisha, utafutaji, malezi, usiri, kukua kwa teknolojia, matarajio ya maisha, sonona, matukio ya nyuma na matumizi ya mihadarati na pombe kupindukia.

Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zinaonyesha kuna ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili kwa asilimia 17 kwa mwaka 2020/21 huku wanaume wakikabiliwa zaidi na tatizo hilo ikilinganishwa na wanawake.

Kati ya wagonjwa wa nje 24,014 walioonwa, wanaume walikuwa 15,205 ikilinganishwa na wanawake 8,809.

Mtaalamu wa Afya ya Akili na Mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Mental Health Tanzania, Dk Philimina Scarion alisema kuna vyanzo vingi vinavyosababisha wanaume wapate msongo mawazo ambao mwishowe hufikia sonona na kujikuta wakipata tatizo la afya ya akili.

“Wanaume wanaoishi katika nchi za uchumi mdogo na kati, kama Tanzania, wengi huwa na msongo wa mawazo mara nyingi ikilinganishwa na wanawake,” alisema Dk Scarion.

Alitaja sababu nyingine kuwa wengi wao ni wazito kuzungumza ya sirini mwao, hivyo hujikuta wakikaa na matatizo moyoni baadaye yanafika hatua ya juu na kuchanganyikiwa.

“Pia, jamii yetu imekuwa na dhana kuwa mwanamume ni mtu mwenye nguvu, hivyo hapaswi kuonyesha udhaifu wa kuumizwa hivyo wanabaki na maswali mengi wakijiuliza na kujijibu wenyewe,” alisema Dk Philimina.

Mtaalamu wa Saikolojia, Saldin Kimangale alitaja baadhi ya sababu hizo ni wanaume kujijengea ukuta na si wepesi kutafuta msaada mapema ukilinganisha na wanawake.

Alisema ongezeko linatokana zaidi na matumizi ya ulevi na dawa za kulevya, tafiti zinaonyesha wanaume ni watumiaji zaidi kuliko wanawake.

“Hilo linachochea wao kupata magonjwa ya matumizi ya dawa za kulevya, pia huchochea kupata magonjwa mengine kama Bipolar, Schizophrenia na magonjwa ya wasiwasi,” alisema Kimangale.

Mwanasaokolojia Charles Kallungu alisema mwanamume huathirika zaidi kwa kuwa ndiye kiungo muhimu cha familia na mtekelezaji wa kwanza, lakini anapokwama kimawazo ni vigumu kutafuta ushauri.

Alisema wengi hudhani anapoomba msaada wa mawazo au kuweka hisia zake wazi ni kuonyesha udhaifu, hii hali imewakumba wengi.

“Wachache wanaojitambua hutafuta msaada wa mawazo, lakini wengi hawapo tayari kusaidika wengine hudhani nikiwa mwanamume sitakiwi kufanya kitu fulani, wengine wanaathirika na matukio ya nyuma aliyoyafanya, hawezi kuongea na mkewe, wengi mwishowe huchanganyikiwa,” alisema.

Malezi

Sababu nyingine inayochochea wanaume kuwa na magonjwa ya akili ni kutokana na malezi.

Kallungu alisema kitu pekee kinachowafanya watoto waathirike ni malezi mabovu yanayosababisha mfadhaiko na sonona.

Yanapotokea hayo mtoto hukosa uhuru wa kujielezea, matunzo sahihi, usimamizi, mahitaji yake muhimu anayakosa na hiyo huanza kumfanya awe na msongo tangu utotoni.

“Si kosa la mzazi wakati mwingine ila ni mazingira, wazazi wengi hawakujiandaa kuwa na watoto ila wamewapata, hii ya kulea watoto huwa inawatatiza baadhi yao ambao hawajakubali uhalisia, kutokukubali uhalisia ni shida huwa inaathiri pia watoto,” alisema Kallungu.

Alisema inapotokea mzazi anakuwa mkali kupitiliza kutokana na msongo wa mawazo alionao, huwa inaleta shida katika makuzi ya mtoto, anakosa uhuru wa kujieleza kwa wazazi wake na humwondolea ujasiri wa kujiamini na hata kufanya vizuri darasani.

“Watoto hukosa uhuru kuwaeleza wazazi yanayowakabili, ndiyo maana kuna kesi nyingi za vitendo viovu vya watoto katika kipindi hiki hasa shuleni, wanaweza kukaa kimya wakaogopa kuwashirikisha wazazi kwa maana kuna hatua ya kwanza ambayo watoto lazima waipate ambayo ni ‘bond’.

Mtaalamu wa Saikolojia, Josephine Tesha alisema wanaume wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya akili sababu ya malezi na jinsi ambavyo jamii yetu inawachukulia.

“Wanaume sio watu wa kuongea au kupenda kuonyesha udhaifu wao. Tokea mtoto mdogo wa kiume akiwa anakuwa anaambiwa “jikaze kama mwanaume” kwa hiyo tangu akiwa mdogo ameshaweka akilini ni jinsi gani anatakiwa kuwa.

“Ili kuwa na afya ya akili iliyo bora unatakiwa uwe unaweza kuongea kuhusu mambo yanayokusibu ili kuyatoa akilini, kama utakuwa unapata matatizo yanasumbua akili na huongei na mtu yoyote ni rahisi kupata msongo wa mawazo, unakuwa na nafasi kubwa ya kupata sonona (depression) na pengine ukapata ukichaa,” alisema Tesha.

Takwimu

Takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili kwa asilimia 17 kwa kipindi cha mwaka 2020/21 huku wanaume wakikabiliwa zaidi na tatizo hilo ikilinganishwa na wanawake.

Kati ya wagonjwa wa nje 24,014 walioonwa mwaka huu, wanaume walikuwa 15,205 ikilinganishwa na wanawake 8,809 ambao ni ongezeko la asilimia 17 ililinganishwa na wagonjwa 20,571 (wanaume 11,560, wanawake 9,011) waliopewa huduma kwa kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2019/20.

Takwimu hizo zimetolewa juzi na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Afya ya Akili, Dk Frank Massao wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakati akipokea misaada ya nguo, viti na fedha kutoka Ecobank.

“Mara nyingi wanaume wanakumbwa zaidi na tatizo la afya ya akili kuliko wanawake, lakini pia kuna ongezeko kubwa la kasi ya maradhi ya akili ukiangalia na namba jinsi inavyopanda hata kwa watoto kati ya 2,163 tuliowapokea mwaka uliopita wa fedha ambao ni chini ya miaka 16, wanaume walikuwa 1,577 na wanawake 586,” alisema Dk Massao ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Afya ya Akili nchini.

Dk Massao alisema hata katika huduma za kulazwa, idara ilitoa huduma kwa watu wazima 1,587 huku wanaume wakiwa 997 na wanawake walikuwa 473.

Alisema wagonjwa waliopitia kwenye kitengo cha marekebisho ya afya ya akili kwa mwaka huu ni 1,673 huku wanaume wakiwa 1,064 na wanawake 609.

Ukubwa wa tatizo

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu alisema idadi ya wagonjwa wa akili imekuwa ikiongezeka, mwaka hadi mwaka.

“Mwaka 2018 tulikuwa na wagonjwa 357,799 waliokwenda kupatiwa matibabu, mwaka 2019 walikuwa 380,000 na mwaka 2020 walifika zaidi ya 500,000,” alisema Dk Ubuguyu.