Sabaya, wenzake kusomewa hoja za awali leo

Aliyekua Mkuu wa wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya(katikati) akiwa na watuhumiwa wenzake wakati wakitoka kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.


Muktasari:

  • Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita leo wanatarajiwa kusomewa hoja za awali ya kesi ya Uhujumu Uchumi inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.


Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita leo wanatarajiwa kusomewa hoja za awali ya kesi ya Uhujumu Uchumi inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Watuhumiwa hao watasomewa mashtaka yao baada ya Septemba 9 mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuipa mamlaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kusikiliza kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi.

Ole Sabaya na wenzake sita wanakabiliwa na mashtaka matano katika shauri hilo.

DPP aliwasilisha hati na ridhaa ya kuruhusu Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tarsila Gervas.

Washtakiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Wakili Tarsila aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, lakini DPP ameona kwa masilahi mapana ya Taifa, kesi hiyo inasikilizwa na Mahakama hiyo ya chini.

Baada ya Wakili Tarsila kuwasilisha nyaraka hizo mbele ya Hakimu Patricia Kisinda, washtakiwa hao walisomewa upya mashitaka hayo ambayo waliyakana.

Makosa yanayowakabili ni kuongoza genge la uhalifu, kosa la pili linalomkabili Sabaya mwenyewe ni kujihusisha na vitendo vya rushwa na la tatu linalomkabili Sabaya ni kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kudaiwa kuchukua Sh90 milioni.

Wakili Tarsila alidai mahakamani hapo kuwa kosa la nne linalomkabili Sabaya ni matumizi mabaya ya madaraka, huku kosa la tano ni utakatishaji fedha.

Washtakiwa wote walikana kutenda makosa hayo. Kesi hiyo inaendelea leo.