Sabaya, wenzake wasubiri hukumu

Muktasari:

  •  Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa ajili ya kusikiliza hukumu ya rufaa yao kupinga kifungo cha miaka 30 jela.



Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa ajili ya kusikiliza hukumu ya rufaa yao kupinga kifungo cha miaka 30 jela.

Mbali na Sabaya waomba rufaa wengine ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura ambao tayari wamefika mahakamani hapo kusikiliza rufaa inayosikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Sedekia Kisanya.

Leo Mei 6,2022 Sabaya na wenzake wamefikishwa mahakamani hapo saa 3:30 asubuhi huku ulinzi ukiendelea kuimarisha kwenye viwanja vya mahakama.

Rufaa hiyo ya jinai namba 129/2021 imeletwa na Sabaya na wenzake hao wakipinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Katika rufaa hiyo waomba rufaa hao wanawakilishwa na mawakili Majura Magafu, Moses Mahuna, Fauzia Mustafa, Sylvster Kahunduka, Edmund Ngemela na Fridolin Bwemelo ambao kwa pamoja walipinga hoja za wajibu rufaa na kuomba mahakama iridhie hoja zao 14 za rufaa na kuwaachia wateja wao huru.

Upande wa Jamhuri (wajibu rufaa) uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali waandamizi Ofmedy Mtenga, Verediana Mlenza na Baraka Mgaya ambao, wanapinga hoja za mawakili wa waomba rufaa na kuiomba mahakama itupilie mbali rufaa hiyo.

Awali Oktoba 15, 2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo aliwahukumu Sabaya na wenzake wawili kifungo cha miaka 30 kila mmoja, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa matatu ikiwamo unyang'anyi wa kutumia silaha.

Wakati akitoa hukumu hiyo, Hakimu Amworo alisema kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa mahakamani, aliridhika washitakiwa hao walimpora Numan Jasin, Bakari Msangi na Ramadhan Rashid.

Hata hivyo, alisema ushahidi ulionyesha kuwa walipowavamia Numan na Ramadhan walitumia nguvu sio silaha lakini, walitenda kosa la unyang'anyi wa makundi na Jamhuri kuthibitisha kosa hilo walipomvamia Msangi walitumia silaha.

Wakati Mahakama Kuu ikitarajiwa kutoa hukumu hiyo leo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha nayo imepanga Mei 31, 2022 kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Sabaya na wenzake sita.