Safari ya Nyerere, kutoka Waziri Kiongozi hadi Waziri Mkuu

Dar es Salaam. Baada ya Chama cha Tanganyika African National Union (Tanu) kushinda uchaguzi na kupata idadi kubwa ya wajumbe katika Baraza la Kutunga Sheria, Mwalimu Julius Nyerere aliteuliwa na Gavana Richard Gordon Turnbull kushika wadhifa wa Waziri Kiongozi.

Nyerere alianza kuutumikia wadhifa huo kuanzia Ijumaa ya Septemba 2, 1960 na alidumu katika wadhifa huo kwa siku 241 hadi cheo kilipopanda tena.

Alipanda cheo na kuwa Waziri Mkuu kuanzia Jumatatu ya Mei 1, 1961. Hiyo ndiyo siku aliyoapishwa kuwa Waziri Mkuu baada ya Tanganyika kupewa Serikali ya mambo ya ndani kabla ya kupata uhuru kamili.

Hata hivyo, Jumatatu ya Januari 22, 1962 Nyerere alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu. Katika vipindi tofauti mwaka 1955 na 1956, Nyerere alikwenda New York, Marekani, kuhutubia Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa Tanganyika.

Mwaka mmoja baadaye, 1957, alitangaza kuwa Tanu ingeshiriki katika uchaguzi wa mwaka 1958 ikiwa tu ungekuwa uhuru na wa haki. Serikali ya kikoloni iliuhakikishia Umoja wa Mataifa kuwa uchaguzi huo utakuwa huru. Huo ndio ulikuwa uchaguzi mkuu wa kwanza kwa Tanganyika.

Kwa mujibu wa kitabu 'Elections in Africa: A Data Handbook' © 1999, uchaguzi wa kuwapata wabunge ulifanyika Jumatatu ya Septemba 8 na Ijumaa ya Septemba 12, 1958.

Mwaka uliofuata uchaguzi wa majimbo yaliyokuwa yamebakia ukafanyika Jumatatu ya Februari 9 na Jumapili ya Februari 15, 1959, kisha ukafanyika mwingine Jumanne ya Agosti 30, 1960.

Jarida la 'Black World/Negro Digest' la Machi 1962 liliripoti kuwa katika uchaguzi wa 1958, wapiga kura waliokuwa wamejiandikisha tayari kwa kupiga kura walikuwa 885,000. Hadi mwishoni mwa Julai, wagombea 58 wa Tanu walikuwa wamepita bila kupingwa na 39 miongoni mwa hao ni Waafrika.

Tanu ilipata viti 12 kati ya 13 vilivyogombewa katika Baraza la Kutunga Sheria. Mgombea mmoja wa Tanu aliyeitwa Chief Amri Dodo alishindwa na mgombea binafsi aliyeitwa Herman Elias Sarwatt katika jimbo la Mbulu.

Katika hotuba yake ya Mei Mosi 1995 katika Uwanja wa Sokoine Mbeya, Nyerere alikiri hivi: “Sasa, mfano mmoja ninaoutumia mwisho kabisakabisa, mwaka 1970 sijui 1971 sijui 1972, eeh! Akatupinga kijana wetu mmoja anaitwa Sarawati katika uchaguzi wa vyama vingi.

“Ulikuwa uchaguzi wa vyama vingi eeh? Ndiyo. Ilikuwa uchaguzi wa vyama vingi. Ilikuwa ni katika uchaguzi wa vyama vingi. Viti vingi sana tulivichukua bila kupingwa. Nadhani hivyo ndivyo ilivyokuwa.

“Katika kiti cha Mbulu tumemweka mtu mmoja anaitwa Chifu (Amri) Dodo. Mwanachama wetu mmoja pale anaitwa Herman Sarawati. Akasema aaah, hiki chama changu hakina akili hata kidogo.

Au viongozi wangu hawana akili. Huyu akiwa na mkoloni ndiye aliyetaka kutufunga sisi ndiye wameonelea awe mbunge wetu katika jimbo la Mbulu?

“Kijana yule akatupinga. Mimi nikatoka hapa Mbeya. Nimesafiri kutoka Mbeya hapa kwenda kumpinga. "Kwenda kumtetea yule candidate (mgombea) wa Tanu. Nikashindwa. Wananchi wa Mbulu pamoja na wanachama wengi tu, wakasema Tanu wamekosea. Wakampa kura Sarawati, mwanachama wa Tanu.

“Anasimama mwenyewe tu. Akatupinga. Ilikuwa haki yake. Mimi nilidhani sasa tunarudisha vyama vingi, tunarudisha na haki zote zile zilizokuwapo za raia, si haki ya kuunda vyama tu, bali pamoja na haki ya private candidate (mgombea binafsi) kusimama akafanya kama chama kinavyofanya.

Kutokana na ushindi wa Tanu katika uchaguzi wa Septemba 1960, ndipo Nyerere akawa Waziri Kiongozi wa Tanganyika, kisha akamteua Derek Bryceson kuwa makamu wake.

Serikali ya kikoloni iliweka masharti kadhaa kwa waliopiga kura katika uchaguzi huo wa mwaka 1958.

Mojawapo ya masharti hayo ni la kuwataka kuwapigia kura (tatu) kutoka kundi la Waafrika, Wahindi na Wazungu.

Legco ambayo iliundwa na Waingereza tangu mwaka 1926, ilikusudiwa kuwajumuisha Wazungu, Wahindi na Waafrika. Vyama vingine vya siasa vilivyoshindana na Tanu katika uchaguzi huo ni Tanganyika United Party (UTP).

Hiki kilikuwa ni chama cha walowezi, lakini kiliungwa mkono na Wahindi wachache na baadhi ya Waafrika.

Kwa kuona utata wa masharti yaliyowekwa na wakoloni kuhusu uchaguzi huo, Tanu kiliitisha mkutano wake wa mwaka uliofanyika mjini Tabora kuanzia Januari 21 hadi 26, 1958, ikiwa ni miezi michache kabla ya uchaguzi huo.

Ajenda kuu ya mkutano huo ilihusu kutafakari juu ya ama kushiriki au kuususia uchaguzi huo.

Masharti mengine ambayo Waingereza walikuwa wameweka ni ili uweze kupiga kura lazima kwanza uthibitishe kuwa una kipato cha pauni 400 za Uingereza kwa mwaka, uwe na elimu isiyopungua darasa la 12 na ajira ya muda wote ambayo inathibitishwa na Serikali ya kikoloni.

Masharti yote haya na mengine yalikuwa na lengo la kuwazuia Waafrika wengi kupiga kura katika uchaguzi huo.

Kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huo kuliwagonganisha sana wajumbe wa mkutano.

Kwenye mkutano huo wajumbe wa Tanu waligawanyika katika makundi mawili, la kwanza likisisitiza chama kishiriki katika uchaguzi na la pili likitaka kuususia.

Mmoja wa waliosisitiza kuususia uchaguzi huo ni Sheikh Suleiman Takadir, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Tanu, na mwingine ni Zuberi Mtemvu, katibu mwenezi wa Tanu.

Wawili hawa walikaribia kabisa kukipasua chama katikati, na walielekea kufanikiwa kama Nyerere asingeingilia kati na kuwashawishi wakubali chama kishiriki katika uchaguzi huo.

Ubishani kati ya Nyerere na Sheikh Takadir kuhusu kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huo ulizidi kiasi kwamba wawili hao walifikia mahali pa kutoelewana na Takadir alivuliwa uanachama wa Tanu.
Wengine waliopinga vikali Tanu kushiriki katika uchaguzi huo ni Jumanne Abdallah na Bhoke Munanka.

Lakini baada ya siku kadhaa za malumbano makali, Nyerere aliungwa mkono na wengi katika mkutano huo, wakiwamo Abdallah Rashidi Sembe, Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Ng'azi Mohammed, Mustafa Shauri na Abdallah Makata, waliokuwa viongozi wa Tanu kutoka mkoani Tanga.

Mkutano huo ulitoa tamko kuwa endapo Serikali ya kikoloni haitahakikisha Tanganyika inapewa uhuru wake bila kuchelewa, Tanu ingewahamasisha wananchi wote wagome nchi nzima. Kwa kauli moja tamko hilo likaitwa "Positive Action".

Pia mkutano huo uliazimia kupinga pendekezo la serikali ya kikoloni la kuitaka Tanu ikubali mpango wa kila mpiga kura awapigie watu watatu, yaani Mzungu, Mhindi na Mwafrika ili kushindana na chama kingine cha siasa cha United Tanganyika Party (UTP), kilichokuwa na matajiri wa kizungu na Kihindi.

Tanu iliibuka na ushindi baada ya kupata viti 28 kati ya 30 vilivyokuwa vinagombewa. Miaka miwili baadaye, ulipofanyika uchaguzi wa wabunge, Tanu ilipata viti 70 kati ya 71 vilivyogombewa.

Kutokana na ushindi huo, Rais wa Tanu, Mwalimu Julius Nyerere, akateuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Tanganyika Ijumaa ya Septemba 2, 1960, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika Jumatatu ya Mei 1, 1961.

Hata hivyo, Jumatatu ya Januari 22, 1962 Nyerere alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu.

Kwa nini alijiuzulu siku chache baada ya Uhuru wa Tanganyika? Ni kweli alijiuzulu kwenda kukijenga chama cha Tanu?
Tukutane toleo lijalo.