Sakata la Gekul bado bichi, THBUT yatia mguu

Mbunge wa Babati mjini, Paulina Gekul

Muktasari:

  • Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB), inataka kupata ukweli wa tuhuma za ukatili na udhalilishaji unaodaiwa kufanywa na Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul dhidi ya Hashim Phillemon.

Unguja. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB), inakusudia kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ukweli wa tuhuma za ukatili na udhalilishaji unaodaiwa kufanywa na Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul dhidi ya Hashim Phillemon, mkazi wa Babati Mjini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 28,2023 mjini Unguja, Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Mohamed Khamis Hamad amesema taarifa za kitendo hicho zimekuwa zikitolewa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, hivyo tume imeamua kufuatilia kwa kina, kupata usahihi.

Amesema pamoja na hatua zilizochukuliwa na mamlaka mbalimbali wameona kuna haja ya kufanya uchunguzi huo kwa mujibu wa ibara ya 130 (1) (c) na (f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977 na kifuungu cha 6 (1) c, f, g pamoja na kifungu cha 15 (1) (a) vya Sheria ya THBUB sura ya 391 ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.

Amesema tukio la Phillemon kudaiwa kukamatwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali katika mwili wake tena katika mazingira ya kazini kwake, ni jambo linalohitaji uchunguzi wa kina.

Amesema Tanzania ni nchi inayoongozwa na  Katiba na kila mwananchi anapaswa kulindiwa heshima yake.

Tuhuma hizo ziliibuka Novemba 25, 2023 baada ya kusambaa kwa video mitandaoni ikimuonyesha Phillemon akielezea kile alochodai ni ukatili na udhalilishaji aliofanyiwa na mbunge huyo.

Wakati hayo yakijiri, inadaiwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho mbunge huyo ni mwananchama wake, kimepanga kukutana na kujadili swala hilo.