Sakata la mchele wa Marekani lamuibua Waziri Bashe

Baadhi ya magunia yaliyobeba mchele huo unaodaiwa kutoka Marekani kuja Tanzania kwa ajili ya msaada.

Muktasari:

  • Asema kuwa ameliambia Shirika lisilo la Kiserikali lililoingiza mchele huo, kuwa Tanzania ina mchele wa kutosha, haikulazimika kuagiza kutoka nje.

Dar es Salaam. Saa chache baada ya kuibuka kwa mjadala katika mitandao ya kijamii juu ya mchele ulioongezwa virutubisho ulioletwa Tanzania kutoka nchini Marekani, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amefunguka akisema waagizaji hawakupaswa kuleta mchele huo kutoka nje, kwa kuwa Tanzania ina hazina ya mchele.

 Akaongeza kuwa kama ni virutubisho, bado shirika lililoagiza mchele huo lingenunua mchele wa ndani na kuwaomba wafadhili wao wauongezee virutubisho hapahapa nchini, huku kila mtu akiona kuliko kuagiza kutoka nje ya nchi.

Mjadala wa mchele huo ulianzia katika mtandao wa X, baada ya ukurasa wa Ubalozi wa Marekani kuweka picha iliyokuwa ikionyesha viroba vya mchele huo, huku ikiambatisha na ujumbe uliosomeka:

"Chini ya mpango wa 'Pamoja Tuwalishe', Wizara ya Kilimo ya Marekani, kwa ushirikiano na Jumuiya za Kimataifa, imetoa msaada wa kwanza wa mchele ulioongezwa virutubisho, maharage na mafuta ya alizeti kutoka kwa wakulima wa Marekani moja kwa moja hadi shuleni katika eneo la Dodoma nchini Tanzania."

Ujumbe huo uliendelea kueleza kuwa msaada huo unalenga zaidi kutoa milo yenye lishe kwa wanafunzi wa shule zaidi ya 300 zinazoshiriki, huku ukieleza kuwa mbali na mchele huo, pia wataanzisha bustani za shule na kufunza mbinu za kuvuna.


Alichosema Bashe

Akizungumzia suala hilo wakati akielezea miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na yale aliyoyafanya katika sekta ya kilimo, Bashe amesema Tanzania inazalisha mchele na maharagwe kwa kiwango cha kutosha.

"Tumewaambia ile NGO, waambieni Wamarekani kuwa mchele upo maharagwe yapo nchi hii, zile fedha wanazotumia kuwapa wakulima wa Marekani wawape Watanzania. Tununue mchele kutoka Tanzania, maharage kutoka hapa Tanzania, halafu hivyo virutubisho mnavyotaka kuweka muwekewe hapahapa Tanzania wote tunaona," amesema Bashe na kuongeza kuwa ameieleza NGO hiyo kuwa Tanzania inajitosheleza kwa chakula.


Maoni mtandaoni

Elisha Mbise alitoa maoni yake katika ujumbe ulio katika ukurasa wa Ubalozi wa Marekani akiandika: "Tanzania tuna chakula cha kutosha...mchele umejaa kila mahali. Walete vitu vya maana, wajenge maabara, walete vifaa vya hospitali, vifaa vya kufundishia, vyuo vya ufundi. Hivi ndivyo vitu vinavyoweza kugusa elimu na afya kama kweli wana nia na kusaidia hayo maeneo.’’

Naye Dani Zayumba aliandika: "Tanzania hatuhitaji chakula cha misaada bali tunahitaji mabadiliko ya mitalaa ya elimu, ili tuweze kujilisha wenyewe. Mnaweza kufananisha mchele wa Mbeya na Marekani kweli?’’