Msaada wa mahindi ya njaa na mbinu za wachache kujineemesha

Muktasari:
Ni taarifa nzuri kwa wananchi hasa wa kipato cha chini na kati baada ya Serikali kutangaza itatoa msaada wa tani 40,000 za mahindi kutoka ghala la chakula la taifa.
Ni taarifa nzuri kwa wananchi hasa wa kipato cha chini na kati baada ya Serikali kutangaza itatoa msaada wa tani 40,000 za mahindi kutoka ghala la chakula la taifa. Taarifa za kutolewa kwa msaada huo zilitolewa miezi miwili iliyopita.
Uamuzi huo unakuja kutokana na kuwapo kwa mfumuko wa bei za vyakula na unga kupanda kutoka Sh700 kwa kilo mpaka Sh1,500 kwa kilo. Hivi sasa kilo moja ya unga ni Sh1,380 mpaka Sh1,400.
Hatua hiyo ya serikali pia inatokana na kuwapo kwa uhaba wa chakula katika baadhi ya mikoa nchini.
Pia hatua hiyo ya Serikali imelenga kuwaokoa wananchi ambao wamekumbwa na tatizo la njaa nchini. Serikali iliweka utaratibu wa kufanikisha msaada huo kwa wananchi, lakini mfumo huo umekumbwa na changamoto nyingi.
Ugawaji mahindi waingia dosari
Wananchi wengi wanailalamikia Serikali wakidai kwamba imekosa umakini katika kusimamia shughuli hiyo na kutoa mwanya kwa mafisadi kujinufaisha huku wananchi wakiendelea kuumia kwa njaa.
Mamalishe Mwajuma Zahoro katika Soko la Karume, anasema njaa ipo na imechangia kupanda kwa bei ya vyakula.
“Ukweli ni kwamba kupanda kwa bei ya chakula kumetuongezea ugumu wa biashara yetu kwa kuwa tumelazimika kupunguza kipimo hicho kutokana na bei tunayonunulia, sisi tunafanya biashara ili tupate faida , lakini sasa manung’uniko ni makubwa,” anasema Zahoro.
Anabainisha licha ya serikali kutoa msaada wa mahindi hakuna mabadiliko yoyote ya bei ya unga.
"Serikali imeshusha bei ya unga baada ya kugawa mahindi, lakini mpaka sasa sijaona mabadiliko," anasema.
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Gervas Kibonge anasema kadri siku zinavyokwenda serikali inakaa mbali na wananchi hasa wenye kipato kidogo.
“Unga wa mahindi ni chakula kinachotumiwa na watu wengi zaidi, licha ya mahindi kuwa chakula kikuu kwa watu wengi, pia ni chakula cha bei rahisi pamoja na maharage, lakini bei ya unga bado iko juu.
"Ajabu ni kwamba siku hizi maharage kilo ni Sh2,500 wakati unga ni Sh1,500, hali hii ni mbaya bei ya sukari nayo iko juu, niliposikia kuhusu mahindi ya serikali nilifarijika kwamba bei itashuka, lakini hadi sasa ipo palepale na inaweza kupanda zaidi," anasema Kibonge.
Kukokana na malalamiko mengi yaliyotolewa na wananchi imebainika kwamba kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya maofisa wa serikali kumesababisha baadhi ya watu binafsi kujinufaisha na msaada huo.
Awali Mkoa wa Dar es Salaam ulipata tani 31,600, lakini mpaka sasa haijulikani kigezo gani kilitumika kugawa msaada huo. Imebainika kwamba baadhi ya wasagishaji walipata mgawo mkubwa zaidi licha ya kuwa na uwezo mdogo wa kusaga nafaka hiyo.
Mmoja wa wasagishaji hao wa Dar es Salaam, John Maganga anasema mashine anayoimiliki inasagisha tani 20 kwa siku, lakini aliambulia tani 15 tu.
Utafiti umebainisha kwamba hakuna vigezo vilivyoainishwa wakati wa kugawa mahindi hayo. Wakati baadhi yao wakishangaa kupewa tani 15 ambazo ni kidogo zaidi wapo waliopewa hadi tani 1,500.
Katika taarifa hiyo inaonyesha kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara hao wamepewa tani hizo 1,500 wakati wana uwezo wa kusagisha tani 30 kwa siku, wakati wapo wengine wenye uwezo wa kusagisha tani 20 kwa siku lakini wameambulia tani 15.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chizza anakiri kuwapo kwa ukiukwaji wa taratibu wa kugawa msaada huo.
Chizza anasema ofisi yake inafuatilia na kwamba mwongozo umetolewa kwa wakuu wa wilaya na mikoa ili kufuatilia ugawaji wa mahindi hayo.
Waziri anasema kuna vigezo ambavyo vinapaswa kutumika wakati wa kugawa mahindi kwa wasagishaji. Wasagishaji hao wanapaswa kuwa na nia na uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Kwa mujibu wa taratibu wasagishaji hao wanatakiwa kuuza unga kwa walaji kwa bei elekezi ya kati ya Sh700 mpaka Sh900 kwa kilo moja na kuzingatia gharama za usafirishaji wa mahindi hayo.
Wakati waziri akisema hayo Diwani wa Kata ya Kiva, Rajabu Kibwana anasema wananchiha hawakupata msaada huo. "Serikali haikuwasaidia wananchi kwa kuwa mtu mmoja alipewa unga chini ya nusu kilo," anasema Kibwana.
Mkazi wa Kijiji cha Kwamsisi, Kata ya Kwamsisi wilayani Handeni anasema kwamba walikuwa wakiuziwa kilo moja ya unga Sh1,000 mpaka Sh1,100 kinyume na bei elekezi ya Sh700 mpaka Sh900.
Katika hatua nyingine, Waziri Chiza anaeleza kwamba wanaamini bei hizo zinawezekana na pia zitakuwa na faida kwa kuwa wanauziwa mahindi hayo kwa bei ya Sh450 kwa kilo, hawapaswi kuyauza bali kusaga na kuuza unga kwa kuzingatia bei elekezi.
“Serikali imeidhinisha kuuzwa kwa tani 40,000 za mahindi kutoka ghala la chakula la taifa na tani 20,000 zitauzwa Januari na Februari, mwaka huu," anasema Waziri Chiza.
Waziri huyo anaeleza viwango vya upatikanaji wa chakula nchini vinatofautiana katika maeneo mbalimbali, wakati mikoa minane yaani Iringa, Mbeya, Kagera, Mtwara, Kigoma, Ruvuma na Morogoro ilikuwa na ziada ya chakula.
Baadhi ya mikoa inayokabiliwa na njaa zaidi ni Manyara, Tanga wilayani Handeni, Shinyanga katika Wilaya ya Meatu, na Mkoa wa Pwani kwenye Wilaya Rufiji. Kutokana na wilaya hizo kukabiliwa na njaa baadhi ya wananchi wamekuwa wakilazimika kula mlo mmoja na wengine kula mizizi ya mimea mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Mikoa saba ambayo ni Pwani, Mara, Tanga, Lindi, Mwanza, Singida, na Dodoma ilikuwa na chakula cha kutosha na mikoa sita, Shinyanga, Tabora, Arusha Kilimanjaro, Manyara, na Dar es Salaam ilikuwa na uhaba wa chakula.
“Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye upungufu wa chakula serikali iliongeza mgao wa chakula cha msaada kutoka tani 18,417.8 hadi tani28,250.300 Januari mwaka huu. Tani 19,040.865 za mahindi zimechukuliwa mpaka sasa," anasema Waziri Chiza.
Jumla ya tani 9,209.435 bado hazijachkuliwa na mikoa iliyopewa mgao wa nyongeza ambayo ni Arusha, Mbeya Tabora, Manyara, Kilimanjaro, na Mara,”anasema.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwapo kwa tatizo la rushwa wakati wa kugawa tani hizo kwa wasagishaji.
Mikoa iliyopewa msaada
Mikoa iliyopendekezwa kupewa mahindi ya mgawo na tani zake kwenye mabano, Arusha (1100)Dodoma (400), Kilimanjaro (400)Lindi (400), Mara(900), Manyara (800), Morogoro (400) na Mwanza (2500).
Mikoa mingine ni pamoja na Shinyanga (1,029)Singida (500), Tabora (1,000), Tanga (700),Mtwara (600), Pwani (700), Simiyu(1971),na Dar es Salaam (6400).
Mahindi hayo yatauzwa kwa wasagishaji kutoka katika mikoa iliyothibitika kuwa na upungufu wa nafaka hiyo.
Wizara ilitangaza utaratibu maalum wa kuuza mahindi kwa wasagishaji waliopo kwenye mikoa ambayo inaaminika kuna nupungufu mkubwa wa chakula.
Kwa mujibu wa taratibu, baada ya mahindi hayo kusagwa yanapaswa kilo moja ya unga inapaswa kuuzwa kwa bei elekezi ya kati ya Sh750 na 900.