Sakata la ndoa ya Dk Mwaka lawagawa viongozi wa dini

Muktasari:

  • Ndoa hiyo ilivunjwa Jumatano iliyopita na Kamati ya Masheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, siku mbili baadaye Baraza la Ulamaa limesema ndoa hiyo haijavunjwa.

Dar es Salaam. Unaweza kusema sakata la kuvunjwa na kusha kurejeshwa kwa ndoa ya Dk Juma Mwaka na Queen Masanja limewagawa watu, huku Baraza la Habari la Kiislamu likimuomba Mufti kuingilia kati.

Baraza hilo la habari limesema linasimama na Alhadi Musa, Sheikh Mkuu wa Mkoa aliyeiongoza Kamati ya Masheikh kuvunja ndoa hiyo kabla ya Baraza la Ulamaa leo kutengua uamuzi huo na kusema ndoa ya wawili hao haijavunjwa.

Jumatano iliyopita, Kamati ya Masheikh ya Mkoa wa Dar es Salaam ilieleza kuivunja ndoa hiyo na kutoa siku 30 za kukata rufaa kabla ya jana Dk Mwaka kuupinga uamuzi huo na kusema ni wa kihuni.
Leo Januari 27, Baraza la Ulamaa lilikutana kwenye kikao cha dharura na kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Masheikh ya mkoa.

Saa chache baada ya uamuzi huo, Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania limezungumza na waandishi wa habari, Magomeni jijini hapa na kueleza uamuzi wa Baraza la Ulamaa unakwenda kuwagawa Waislamu.

"Mufti tunakuomba uingilie kati, Sheikh Mkuu wa Mkoa ni wako na Bakwata pia ni yako, kitendo cha Baraza la Ulamaa kutengua uamuzi wa Sheikh Mkuu, maana yake ni nini? Kwamba hakutoa uamuzi sahihi au?" amehoji Mwenyekiti wa Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania, Sheikh Said Mwaipopo.

Amesema kitendo cha Dk Mwaka kuuita uamuzi wa masheikh ni wa kihuni, yeye ndiye alipaswa kuchukuliwa hatua na si Baraza la Ulamaa kutengua tena uamuzi wa Kamati ya Masheikh wa mkoa.
"Tena anapaswa kuomba radhi, aonyeshe uhuni wa masheikh ni nini? halafu atueleze kama yeye ni msafi, ajitafakari na angeweza katika hili jambo angekaa kimya, yeye si wa kwanza kuachwa.
"Mwanamke ameshasema hakutaki, muache labda amepata mtu anayeendana nae, au tabia zako hazifai" amesema Mwaipopo.
Amemuomba Mufti kuingilia kati sakata hilo kwa maslahi ya dini, kwani liko chini yake na wote waliotofautina katika uamuzi, Baraza la Ulamaa na Kamati ya Masheikh wa Mkoa ni watu wake.
Mwanaharakati huru wa Kiislamu, Hussein Msopa 'Sharifu Majini' amesema amesema Baraza la Ulamaa lilipaswa kumuacha Dk Mwaka aende mahakamani na si kutengua uamuzi wa awali wa kuivunja ndoa hiyo.
"Mwaka unachotakiwa  ni kwenda mbele sio Baraza la Ulamaa kurudisha uamuzi chini, inawezekanaje taasisi moja, hawa wanabatilisha na hawa wanahalalisha?
"Tunaamini talaka ya Queen ipo palepale, kwani uamuzi wa kuirudisha umevunja katiba ya Bakwata kifungu cha ya 48," amesema.