Prime
Samia acharuka siri nyeti kuvuja, bosi Tanesco ana kazi maalumu

Muktasari:
- Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na wimbi la nyaraka mbalimbali zenye mihuri inayodaiwa kuwa ni ya Serikali kwenye mitandao ya kijamii, jambo linalozua sintofahamu licha ya baadhi kutolewa ufafanuzi na kukanushwa.
Dar es Salaam. Suala la maadili kwa watumishi wa umma wa kada mbalimbali limeendelea kuwa changamoto kubwa kwa Taifa. Hilo linatokana na kuwepo kwa baadhi ya viongozi na watumishi wanaokwenda kinyume na miiko iliyowekwa, hivyo kusababisha athari kwenye utendaji na huduma kwa wananchi.
Kutokana na hilo, Rais Samia Suluhu Hassan ameliagiza Baraza la Maadili kusimamia utendaji wa watumishi wa umma, kwa kuwa ndiyo injini ya uendeshaji wa nchi.
Rais Samia, amesema kwa kuwa viongozi ni binadamu, lakini pia wamewekewa miiko, na kwamba endapo tathmini itafanyika, huenda ni asilimia 30 pekee ndiyo wanaofuata miiko ya uongozi.
“Nendeni mkasimamie maadili kwenye utumishi wa umma. Tumeharibika. Leo hii mtumishi wa umma anakosa uzalendo, anakosa moyo na kuthubutu kuchukua nyaraka ya siri kwenye mafaili, kupiga picha kwenye simu yake na kusambaza… Akijua anamkomoa Rais, kumbe ni yeye ndiye amekosa maadili. Hawajibiki kwa taifa lake, uzalendo kwa taifa lake hakuna.
“Hilo ni moja, lakini kuna mengi ndani ya utumishi wa umma, katusaidieni, kwani utumishi wa umma ndiyo injini ya uendeshaji wa nchi,” amesema Samia.
Rais Samia amesema hayo leo Jumamosi, Mei 24, 2025, wakati akiwaapisha viongozi aliowateua kwa nyakati tofauti, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Fred Msemwa, na Naibu Katibu wa tume hiyo, Dk Blandina Kilama.
Wengine walioapishwa ni Profesa Tumaini Nagu kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), anayeshughulikia afya, na Jaji John Mgeta, aliyeapishwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Maadili.
Baada ya kuwaapisha, amewataka viongozi hao kwenda kushirikiana na watu watakaowakuta katika maeneo yao ya kazi, huku akitoa rai kwa waliopo katika ofisi hizo kuwapa ushirikiano wa kutosha.
Kauli ya Rais Samia inakuja wakati kukiwa na wimbi la kuchapishwa kwa kile kinachodaiwa kuwa nyaraka za Serikali kwenye mitandao ya kijamii, huku zikiwa na nembo ya siri.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mara baada ya tukio la uapisho Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Mei 24, 2025.
Hata hivyo, zipo baadhi ya nyaraka zinazosambaa mitandaoni, ambapo mamlaka husika tayari zimejitokeza kukanusha.
Lakini, katika kuonyesha kuwa uvujaji wa nyaraka za Serikali ni janga kubwa, Rais Samia amekuwa akikemea suala hili mara kwa mara anapozungumzia utumishi wa umma.
Novemba 22, 2022, akiwa katika mkutano mkuu wa 10 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), Rais Samia aliwataka kutunza siri za Serikali kwa uadilifu na weledi, kwani wasipofanya hivyo, watadhulumu haki za watu.
Alipokuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi, Novemba 29, 2024, naye aliwahi kukemea kitendo cha baadhi ya watunza kumbukumbu serikalini kuvujisha siri katika maeneo yao ya kazi, na kuwataka kuzingatia maadili ya kazi yao.
“Niwaombe mzingatie utunzaji wa siri, kwani kumekuwa na matukio ya barua za vibali vya uhamisho kuvuja kupitia masijala kabla ya kuifikia taasisi husika na mlengwa, au taarifa za mtumishi anayepata uhamisho wa ndani kuvuja katika taasisi yake kabla ya yeye mwenyewe kupata barua ya uhamisho wake. Hivyo, muache tabia hiyo ambayo ni kinyume na taratibu za kiutumishi,” alisema Ndejembi.

Viongozi wateule wakiapa kiapo cha maadili kwenye hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Mei 24, 2025.
Aprili 29, 2024, Kaimu Mkurugenzi anayesimamia mafunzo kwa watumishi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Sijali Korojelo, alisema kuna mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma, ambao unafanya baadhi yao kuvujisha nyaraka za siri.
“Ipo shida ya uvujaji wa siri za Serikali. Siku hizi ni kawaida kukuta barua za siri kwenye mitandao ya kijamii, na ndio maana tumeona tuwakumbushe juu ya umuhimu wa kutunza siri za Serikali na madhara yake kama watabainika,” alisema katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya siku mbili kwa maofisa tarafa na watendaji kata wa halmashauri sita za Mkoa wa Geita.
Changamoto hii haipo Tanzania Bara pekee, bali hadi Zanzibar wanapambana nayo. Machi 27, 2025, Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Uendeshaji wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Rashid Makame Hamdu, aliwataka watumishi kufuata sheria za kazi kwa kutunza nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji, ili kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
“Iwapo wafanyakazi watafuata sheria za utumishi wa kazi kwa kutunza nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji, kutasaidia kujiamini katika utekelezaji wa majukumu yao na kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema Rashid.
Bosi Tanesco ana kazi maalumu
Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange, amepewa maagizo maalumu na Rais Samia, akitakiwa kusimamia na kukamilisha miradi yote ya umeme.
Pia, Twange ametakiwa kwenda kusafisha makando makando yote ndani ya shirika hilo kubwa nchini.
“Katika mchujo mkubwa tuliangalia uwajibikaji, uzoefu, na mambo yote. Umeibuka kuwa unaweza kushika shirika hili. Shirika hili ni security (usalama) ya nchi, kwani umeme ndani ya nchi yetu ndiyo kila kitu,” amesema Samia.
Amemtaka kufikiria mfano wa umeme kuzimwa maeneo ya wananchi kwa siku mbili au tatu, kelele ya kisiasa itakayopigwa na pia afikirie upande wa pili ambapo katika maeneo ya kiuchumi, kukosekana kwa umeme kunaweza kuzorotesha shughuli zote.
“Tumefanya jitihada kama Serikali kuweka uzalishaji umeme katika vyanzo kadhaa…”
Amesema chanzo kikubwa kwa sasa ni Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), ambalo ni roho ya nchi, kwa kuwa awali asilimia 60 ya umeme ulikuwa unatokana na gesi, lakini sasa utatokana na vyanzo vingine baada ya JNHPP kuanza kazi.
“Tuna umeme wa kutosha. Chalinze tunaingiza umeme. Tatizo tulilonalo ni usafirishaji kwenda Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini. Miradi hiyo ipo, lakini kumekuwa na kusuasua kuanza utekelezaji wake.
“Hivyo, ukaangalie na kuhakikisha usafirishaji unafanyika kupeleka umeme kutoka kwenye gridi sehemu hizo,” ameagiza Rais Samia.
Pia, amesema vipo vyanzo vidogovidogo vinavyotoa umeme maeneo mbalimbali ya Tanzania, hivyo vitupiwe jicho vizuri, kwani kumekuwa na ongezeko la uwekezaji nchini na viwanda vikihitaji umeme wa uhakika ili vizalishe.
Amesema huko mbele pia ni vyema kuangalia suala la nishati jadidifu, ambapo nchi imekuwa ikishughulikia umeme jua, upepo, lakini Tanzania ina madini ya uranium.
“Sasa ni vyema kusimamia mradi wetu wa Tunduru. Wale wawekezaji waanze kazi na tufaidike na rasilimali ile. Kwanza tufaidike ndani ya nchi, na makadirio pale ni kama tani 58,500 zipo. Wakianza kuchimba na ugunduzi katika eneo hilo, wanaweza kupata nyingi zaidi,” amesema Samia.

Viongozi wateule wakiapa kiapo cha maadili kwenye hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Mei 24, 2025.
Amesema ni muhimu mradi huo uanze, kwani unaweza kufanya nchi kuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi ya ndani na kuuza nje ya nchi, kama ilivyo sasa kwa Zambia, na huenda ikailazimu Tanzania kuacha kununua umeme kutoka Ethiopia.
“Tumefanya jitihada kupeleka umeme vijijini, kwani Ilani ilitaka mwaka 2025 vijiji vyote viwe vimepata. Sasa vijiji vyote 12,318 vina umeme. Nguvu inawekwa katika vitongoji na huko asilimia 52 tayari vina umeme. Kazi inaendelea katika vitongoji 2,000. Tukimaliza, tutakaribia lengo tulilowekewa,” amesema.
Kuhusu nishati safi ya kupikia, amesema ni suala linalogonga sehemu mbalimbali. Kadri usambazaji wa umeme utakavyofanyika vijijini, watachangia kufikiwa kwa lengo la asilimia 80 ya Watanzania kuachana na matumizi ya nishati chafu ifikapo mwaka 2034.
Pia, amemtaka Twange ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, kwenda kusimamia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme, ili kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika.
“Kubwa zaidi ndani ya shirika lako, nenda kasafishe makando makando yaliyopo katika kutoa umeme. Nilimuona Naibu Waziri Mkuu (Dk Doto Biteko) kaenda, alizunguka, hakufurahishwa na mambo aliyoyakuta katika maeneo mengine. Nenda kasimamie,” amesema Rais Samia.
Maagizo kwa Profesa Nagu
Rais Samia amemtaka Profesa Nagu kusimamia hospitali na vituo vya afya vilivyo chini yake, kwani Serikali imefanya kazi ya kupeleka vifaa tiba, vitendanishi na wataalamu, na bado wanaendelea kupeleka, huku akikiri kutambua changamoto zilizopo.

Profesa Tumaini Nagu akila kiapo kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Mei 24, 2025.
Pia, amesema Serikali inaendelea na ukarabati wa hospitali kongwe ambazo wanataka zifanane na zilizojengwa hivi karibuni, sambamba na kuzipatia vifaa vya kisasa.
“Kasimame vyema kwa sababu nafasi yako hiyo kuna kushirikiana na wanasiasa, hasa wabunge na madiwani. Wao wana changamoto zao, kasimame vyema, shirikiana nao kutatua changamoto wanazoleta. Linalowezekana, waambie ‘tunaweza, tutafanya’, kawaone, kawatembelee, na lisilowezekana wape sababu za maana,” amesema.
Pia, amemtaka kujitahidi kutafuta ufumbuzi wa shida za wananchi na kuondoa urasimu usiokuwa na tija katika mchakato wa manunuzi, na kuzingatia sheria.