Samia alivyojenga umoja akiipitisha nchi salama kwenye nyakati ngumu

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe (kushoto) pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana (kulia) mara baada ya kupokea taarifa ya Maendeleo ya mazungumzo ya mchakato wa maridhiano ya kisiasa, Ikulu Jijini Dar es Salaam juzi. Picha ya Ikulu


Ni safari ya milima na mabonde, kupanda na kushuka. Hivyo ndivyo unavyoweza kuielezea kwa ufupi miaka mitatu madarakani ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Lakini, pamoja na yote hayo unaweza kusema imekuwa safari ya neema kwa Watanzania kutokana na kazi kubwa aliyoifanya kulijenga Taifa na kuirudisha Tanzania kwenye ramani ya matumaini katika nyanja tofauti.

Rais Samia aliingia madarakani tarehe kama ya leo (Machi 19, 2021) akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, hayati John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu ya moyo.

Baada ya kuingia madarakani, Rais Samia alilikuta Taifa likiwa limegawanyika kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara kuzuiwa (isipokuwa kwa madiwani na wabunge waliochaguliwa kufanya hivyo majimboni mwao), mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji yakiwa yametetereka.

Pia kuwapo kwa matukio ya watu kupotea ama kutekwa na watu wasiojulikana. Hata hivyo, mamlaka za Serikali kwa nyakati tofauti zilikuwa zinaeleza kuyafanyia kazi matukio hayo.

“Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu, kufarijiana, kuonyesha upendo, kuenzi utu wetu na uzalendo wetu tukiwa pamoja. Ni wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, kwa matumaini na kujiamini.”

“Si wakati wa kutazama yaliyopita ni wakati wa kutazama yajayo, si wakati wa kunyoosheana kidole, ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele, kufutana machozi na kufarijiana ili kuweka nguvu pamoja na kujenga Tanzania mpya,” alisema Rais Samia, Machi 19, 2021, mara tu baada ya kuapishwa Ikulu.

Katika miaka mitatu, aliunda Serikali yake kwa kuendelea na sehemu kubwa ya mawaziri waliokuwepo wakati wa Serikali ya awamu ya tano, huku akitoa maelekezo ya namna anavyotaka wafanye kazi kuwatumikia wananchi.

Jambo muhimu alilolifanya baada ya kuingia madarakani, ni kujenga umoja wa kitaifa. Wakati huo, Taifa lilikuwa limegawanyika kwa misingi ya kiitikadi, jambo ambalo lilihatarisha amani na ustawi wa Taifa hili.

Amekuwa akishiriki shughuli za kijamii, kisiasa na kiutamaduni kwa lengo la kujenga umoja wa kitaifa. Mfano, amekuwa akiongeza hamasa kwenye timu za mpira wa miguu hasa timu ya Taifa na vilabu vya Simba na Yanga vinaposhiriki kwenye mashindano ya kimataifa.

Serikali yake imekuwa ikitoa Sh5 milioni na Sh10 milioni kwa kila goli linalofungwa, lengo ni kuzipa hamasa timu hizo katika mashindano ya kimataifa, jambo ambalo limeongeza umoja kwa Watanzania kupitia michezo.

Pia, aliunda Tume ya haki jinai kwa ajili ya kupitia mifumo ya utoaji haki nchini na Tume hiyo ilifanya kazi kwa kupokea maoni ya wadau mbalimbali na kuyawasilisha kwake, ikiwa na mapendekezo maalumu kwa ajili ya kuboresha eneo hilo.

“Hali ilikuwa mbaya sana, watu walikuwa wanachukuliwa na hawaonekani tena, tunasikia maiti zimeokotwa baharini kwenye viroba. Watu walikuwa na vidonda mioyoni mwao na hiyo ilisababishwa na siasa za wakati ule,” anasema Malik Ngalisa, mkazi wa Pugu, Dar es Salaam.

Katika miaka mitatu, Rais Samia amefanikiwa kurejesha imani ya wawekezaji ambao walikuwa wakifunga biashara zao na kukimbilia mataifa mengine, kutokana na hofu ya kunyang’anywa fedha zao au kubambikiwa kodi isivyo halali.

Kazi kubwa aliyoifanya Rais Samia ni kuwahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya biashara, huku akitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutowabambikia kodi wafanyabiashara, bali wakusanye kodi kwa haki.

Vilevile, Rais Samia alifungua milango ya demokrasia hapa nchini. Itakumbukwa Juni 2016, hayati Magufuli alitangaza marufuku ya mikutano ya hadhara, lakini Januari 3, 2023, Rais Samia aliondoa marufuku hiyo.

Alianzisha falsafa ya 4R kwa maana ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya kwa lengo la kuwaunganisha Watanzania na kuboresha mazingira ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

“Kwangu binafsi nadhani Rais anafanya jambo jema kuja na falsafa ambayo inaongoza na sisi tutaitumia kwa kuonyesha hatua zinazopigwa lakini pia kwa kukosoa kutokana na misingi ambayo imewekwa,” alisema Zitto Kabwe, kiongozi wa zamani wa ACT Wazalendo.


Azichambua 4R

Mhadhiri na mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe alitoa tathmini yake kuhusu R4 za Rais Samia akisema kwa sehemu kubwa amefanikiwa hasa katika kulileta Taifa pamoja.

“Utakumbuka Rais wetu alichukua hatamu za uongozi wa nchi yetu kipindi ambacho mshikamano wetu kama Taifa kwa upande wa siasa ulikuwa umeanguka, kipindi ambacho siasa za upinzani zilionekana kama uadui na kuondoa dhana nzima ya lengo kuu la kurejesha siasa za vyama vingi mwaka 1992,” anasema Dk Kabobe.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya Katiba na siasa nchini, Deus Kibamba alisema Rais alikuwa na nia ya kuwapatia Watanzania Katiba mpya na alikuwa anahitaji kuungwa mkono na wasaidizi wake, lakini kwa bahati mbaya wamemsaliti.

Rais Samia ameongeza chachu ya ushiriki wa wanawake kwenye vyombo vya uamuzi, huku akiongeza uteuzi wa wanawake kwenye nafasi za kisiasa serikalini na mashirika au taasisi za Serikali.

Katika uongozi wake idadi ya wanawake kwenye taasisi za umma, vyama vya siasa, kampuni za biashara, bodi za mashirika, Baraza la Mawaziri, wakuu wa mikoa na sehemu nyingine ngazi ya chini imeongezeka.

“Tumepiga hatua katika suala ya jinsia ndani ya hii miaka mitatu, hatujafikia usawa wa 50 kwa 50. Tunahitaji kuongeza ushiriki wa wanawake hili siyo jukumu la Rais pekee, bali ni jamii nzima,” anasema mwanaharakati, Dk Hellen Kijo-Bisimba.




Nyakati ngumu zilizomkabili

Kupanda kwa gharama za maisha ni moja ya mambo ambayo yameongezeka zaidi wakati wa utawala wake kutokana na kupaa kwa bei za bidhaa za vyakula hususani sukari, mafuta, vifaa vya ujenzi na mahitaji mengine muhimu ya kibinadamu.

Serikali yake imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuweka ruzuku kwenye bei ya mafuta, kutangaza bei elekezi kwenye sukari.

Hata hivyo, wananchi bado wanakabiliwa na gharama kubwa za maisha. “Uchumi haujengwi kwa siku moja ni mchakato. Kwa hatua anazochukua Rais zikiungwa mkono zitapunguza hali ya umasikini wa watu,” anasema Dk Revocatus Kabobe.

Upatikanaji wa umeme na maji wa uhakika pia ni changamoto anayokabiliana nayo katika utawala wake. Hata hivyo, Shirika la Umeme (Tanesco) limewasha mtambo mmoja kati ya tisa katika bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na kuingiza megawati 235 kwenye gridi ya Taifa ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Licha ya kuwepo kwa mipango mbalimbali ya kutatua changamoto hizo, bado hajafanikiwa kuboresha huduma hizo muhimu za kijamii. Hata hivyo, tatizo la kukatika kwa umeme linalokwamisha upatikanaji wa maji pia limepungua.

Vilevile, kutokea kwa maporomoko ya udongo katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara ambayo yalisababisha vifo vya watu 89, uharibifu wa makazi, miundombinu na mali yakiwamo mazao.

Hata hivyo Rais Samia alionyesha kuimudu vema changamoto hiyo, ikiwamo kutoa tumaini la kuwajengea nyumba za Sh25 milioni au Sh30 milioni ili warudi kwenye makazi yao.

Samia alitoa tumaini hilo mjini Dodoma Desemba 10,2023 alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali Ikulu Chamwino, baada ya kupokea hundi ya Sh2 bilioni kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kusaidia maafa hayo. Pia Serikali ilitoa Sh1 milioni kwa kila maiti iliyotokana na maporomoko hayo.

Vifo vya viongozi wastaafu katika utawala wake ni moja ya nyakati ngumu alizokabiana nazo. Februari, mwaka huu, vimetokea vifo vya viongozi wastaafu wa kitaifa ambao ni Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa aliyefariki Februari 10, 2024 na Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyefariki Februari 29, 2024.

“Nampongeza Rais Samia kwa kusimamia vizuri mazishi ya kitaifa ya viongozi hawa. Kama mfariji wa Taifa alitimiza jukumu lake kikamilifu. Tunampa pole kwa kuunguliwa na maktaba hizo kama anavyoziita mwenyewe,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie.