Mbowe afichua alichoteta na Rais Samia

Muktasari:

  • Mbowe ametaja mambo aliyozungumza na Rais Samia muda mfupi baada ya kutoka mahabusu kuwa ni pamoja na kumtaka asirithi ukatili wa mtangulizi wake, kutaka wafungwa wa kisiasa waachiwe na kusimamia haki ikiwemo kuruhusu mikutano ya hadhara.

Mwanza. Huenda ukawa ni miongoni mwa watu wenye kiu ya kutaka kujua Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alizungumza kitu gani na Rais Samia Suluhu Hassan muda mfupi baada ya kuachiwa kutoka gerezani.

 Akihutubia wakazi wa Kata ya Kakonko Mjini mkoani Kigoma, Mbowe aliyekaa rumande kwa zaidi ya siku 240 akikabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo la ugaidi kisha kufutiwa mashtaka hayo Machi 4, 2022 amefunguka mambo aliyoteta na Rais Samia.

"Asubuhi nilikuwa mfungwa jioni Ikulu. Nilimwambia Rais Samia wewe ni mwanamke na siku zote katika jamii ya binadamu, mlezi wa familia ni mama; nikamwambia mama jiepushe usirithi ukatili wa mtangulizi wako kwa sababu nchi hii ina kilio," amefichua Mwenyeki huyo

"Jambo la pili nilimwambia wakristo tunakiri maandiko matakakatifu yanayosema Haki huliinua Taifa lakini dhambi ni aibu kwa wote. Sijaja kuomba cheo lakini nimekuja kukwambia kwamba Serikali ya chama chako iliiba kura zetu lakini ilishindwa kuiba mapenzi na imani ya wananchi kwa Chadema," amesema.

Aidha, Mbowe alimwambia Rais Samia kwamba hatoweza kuiongoza nchi kwa kuitenga Chadema kwani nusu ya watanzania ni wanachama wake, badala yake washirikiane kurekebisha madhaifu yaliyojitokeza.

"Ukijenga haki katikati ya CCM ni kuwapunguzia mamlaka na wao hawataki inahitaji busara na hekima kukabiliana nao. Kadri tunavyokwenda tunaona wanazidi kulegeza," Amesema.

Pia amesema tangu afanye mazungumzo na Rais Samia, wafungwa wa kisiasa wanaotokea Chadema walikuwa zaidi ya 470 tangu uchaguzi wa 2020 lakini hadi kufikia leo Mei 18, 2023 wamebaki wafungwa watatu.

"Watu waliuwawa, wengine walibambikiwa kesi za kubaka na wengine walikimbilia uhamishoni. Sasa hivi tunaendelea kuangalia namna bora ya kuwaondoa wafungwa wale gerezani," amesema Mbowe.

Amewatia moyo watanzania na kuwataka wasikate tamaa kwa kile alichodai shughuli ya kuondoa CCM madarakani siyo nyepesi inahitaji kujitoa sadaka kama alivyofanya katika kipindi cha miaka saba tangu 2015.

Chadema inaendelea na mikutano ya hadhara ambapo leo imefanyika katika kata nne za wilaya ya Kakonko huku kesho ikiendelea katika kata nne za wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.