Samia ataja sababu kukubali PhD ya tatu ya heshima

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ameweka wazi sababu za kukubali kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Usimamizi wa Utalii na Masoko ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema sababu za kukubali kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima ya Usimamizi wa Utalii na Masoko ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kuwa ni pamoja na kuimarisha utalii wakati akiwa Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Utalii.

Ameeleza hayo leo Desemba 28, 2023 mjini Unguja, muda mfupi baada ya Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi kumtunuku shahada hiyo katika mahafali ya 19 yaliyofanyika chuoni.

Katika hotuba yake, Rais Samia bila kutaja siku, amesema alipopokea barua iliyoelezea nia ya yeye kutunukiwa shahada hiyo ilibidi awatafute baadhi ya watu aliofanya nao kazi alipokuwa Wizara ya Utalii na walimpa sababu za kukubali kutunukiwa shahada hiyo ikiwemo kuimarisha utalii.

Ameeleza alipokuwa akihudumu katika wizara hiyo, alishirikiana na wenzake kuanzisha Baraza la Biashara Zanzibar ambalo kwa mara ya kwanza mwenyekiti alikuwa Rais Amani Abeid Karume na ndani ya miaka mitano walikuza biashara.

Pia amesema walimkumbusha jinsi alivyoimarisha uhusiano ya sekta ya umma na binafsi katika utalii, na alivyochochea uwekezaji wa hoteli zenye majina makubwa ikiwemo Kempiski, Zuri Residence aliyoipa kibali cha ujenzi.

Amesema akiwa wizara hiyo walitumia mwezi mmoja kuzunguka mabara tofauti duniani kuitangaza Zanzibar kama kituo kizuri cha utalii ikiwa ni ruhusa ya Rais Aman Abeid Karume.

“Tulikwenda Uarabuni kuitangaza Zanzibar, Finland, Norway na Sweden kote kuisemea,” amesema.

Kuanzishwa kwa mchakato wa kurekebisha bustani ya Forodhani na kusimamia vizuri sekta ya utalii katika kipindi kigumu cha mdororo wa uchumi mwaka 2018 ni moja ya kitu kilichotajwa kuwa sababu ya kupewa shahada hiyo.

“Kipindi kile kuliibuka homa ya mafua, hivyo ilitulazimu kudhibiti taarifa za ugonjwa huo zisienee ili watalii waendelee kuja,” amesema.

Ametaja pia filamu ya Royal Tour aliyoifanya ikiwa ni mikakati ya kuitangaza nchi kupitia vivutio vya utalii vilivyopo.

“Wakati tunafanya yote haya dhamira yetu ilisukumwa na kulenga kuwaletea maendeleo wananchi na kuimarisha ustawi wao, hatukuwaza kuwa ipo siku jitihada hizo zitaonekana na kupewa heshima hii,” amesema Samia.

Amesema shahada hiyo ni mahusus kwa Watanzania wote wanaompa moyo na ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake akiwa mkuu wa nchi, watu wanaoifanya kazi katika sekta ya utalii na Rais mstaafu za Zanzibar, Abeid Aman Karume kutokana na malezi yake.

Ametumia nafasi hiyo kuwaasa wahitimu kutumia elimu zao kuleta mabadiliko chanya katika jamii, pindi wanaporudi majumbani na kuwataka kutambua wanapokwenda kuna changamoto nyingi za kimaisha, hivyo ni vyema kukabiliana nazo.

“Mawazo yenu yawe mema ukijiwazia mabaya moyo, mdomo kila kitu kitakuwa kinabeba mabaya,” amesema.

Pia ameeleza kufurahishwa na wingi wa wanawake waliohitimu chuoni hapo ambao ni asilimia 58 ya wahitimu wote, huku akieleza hayo ni matokeo makubwa ya Serikali ya Zanzibar. Amesema wakati akisoma, kadri darasa lilivyoongezeka ndiyo wasichana walipungua.

“Hivyo hii asilimia 58 Serikali imefanya kazi kubwa, nawapongeza,” amesema Samia.

Kabla ya kumkaribisha Rais, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa amesema Rais Samia alistahili kupewa hadhi ya Profesa kutokana na uthubutu alioonyesha katika uongozi, ukomavu na uvumilivu wa kisiasa.

“Niliuliza wakati linakuja wazo la kupewa PHD kwani haiwezekani kupewa Profesa moja kwa moja? Wakasema kuna taratibu zake, lakini tutalishughulikia," amesema Lela.

Hii ni mara ya tatu Rais Samia kupewa udaktari wa heshima tangu awe Rais. Mara ya kwanza aliupata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Novemba 30, 2022.

Baadaye Oktoba 10, 2023 alitunukiwa Shahada ya Heshima ya pili ya Udaktari wa Falsafa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru kwenye hafla iliyofanyika jijini New Delhi ambayo aliiekeza kwa wasichana wote wa Tanzania.