Samia ataka viongozi wapya watangulize matokeo, uadilifu
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza leo Jumatatu Julai 27, 2026, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar, wakati wa hafla ya kuwaapisha naibu makatibu wakuu na viongozi wengine wa taasisi za umma walioteuliwa wiki iliyopita.
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amewaapisha viongozi wapya wa Serikali na kuwataka kuongoza kwa uadilifu
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaapisha viongozi wapya aliowateua katika nafasi mbalimbali za Serikali na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji, ushirikiano na utoaji wa matokeo yanayogusa maisha ya wananchi.
Rais Samia ameeleza hayo leo Jumatatu Julai 27, 2026, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar, wakati wa hafla ya kuwaapisha naibu makatibu wakuu na viongozi wengine wa taasisi za umma walioteuliwa wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, Rais Samia amesema uteuzi huo unaonesha imani ambayo Serikali imewawekea viongozi hao, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kujituma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Rais Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dk Latifa Khamis kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar.
Amemtaka Dk Latifa Mohammed Khamis aliyeapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, kuimarisha usimamizi wa masuala ya Muungano na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi ili kuendeleza umoja na mshikamano.
"Katika eneo la mazingira, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha juhudi za uhifadhi huku hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zikipewa kipaumbele," imeeleza taarifa hiyo.
Viongozi wateule wakiapa kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kwenye hafla iliyofanyika leo Jumatatu Julai 27, 2026 Ikulu ya Tunguu Zanzibar.
Kwa upande wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ameelekeza kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Katika sekta ya uchukuzi, Rais Samia ametaka kuharakishwa kwa utekelezaji wa miradi ya reli, barabara, bandari na usafiri wa majini.
Pia, ametaka kufanywe tathmini endelevu ya utendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Maelekezo mengine, aliyatoa kwa Wizara ya Katiba na Sheria, akiitaka iimarishe upatikanaji wa haki kwa wananchi kupitia kampeni za msaada wa kisheria.
Rais Samia Suluhu Hassan akimuapisha Prisca Lwangili kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar.
Rais Samia, ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kuongeza juhudi za kutafuta masoko mapya na kuimarisha maonesho ya biashara kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi.
Pia, amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), kuimarisha ulinzi wa rasilimali za utalii na wanyamapori, akibainisha kuwa, sekta hiyo ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato ya Taifa.
Aidha, ameliagiza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuendelea kujijenga kama chombo cha umma kinachotoa taarifa zenye masilahi ya Taifa kwa kuzingatia weledi, ubora wa maudhui na mahitaji ya wananchi.
Walioapishwa katika hafla hiyo ni Dk Latifa Mohammed Khamis, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Prisca Lwangili, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Ephraim Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade.
Wengine ni Salum Mnali aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Massana Mwishawa aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa na Asha Mbaruk aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).