Samia atangaza kuwa mdhamini ligi ya kwaya za Utumishi, Bunge na Mahakama

Muktasari:

  • Baada ya kufurahishwa na ujumbe kwenye wimbo ulioimbwa na kwaya ya Mahakama na hasa kuhusu haki, ametangaza kuwa mdhamni wa ligi ya kwaya.

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa mdhamini wa ligi ya kwaya itakayohusisha kwaya tatu za mihimili mitatu-- Serikali, Mahakama na Bunge.

 Rais Samia amesema hayo le Alhamisi, Februari mosi, 2024 wakati akihutubia  kwenye kilele cha Siku ya Sheria nchini.

Miongoni mwa maneno yaliyosikika kwenye wimbo ulioimbwa na kwaya ya Mahakama kwenye sherehe hizo ni kwamba haki iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu sasa inatolewa kwa wakati na watu wanatoka haraka mahakamani.

“Haki ikitolewa kwa wakati hueneza amani, uchumi, utulivu na usawa,” ulisikia ujumbe wa kwenye sehemu ya wimbo huo ambao pia ulikuwa na ujumbe uliowataka wadau wote wa Mahakama kutenda haki wakiwamo polisi, magereza, waendesha mashitaka na kwamba  umuhimu wa haki jinai ni kwa ajili ya ustawi wa haki.

Rais Samia amesema amezungumza na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akitaka kudhamini ligi ya kwaya kwa kuzihusisha kwaya za Utumishi wa Umma, Bunge na Mahakama.

Amewataka kujipanga wenyewe na yeye atakuwa mdhamini wa ligi hiyo.

Kwaya ya Utumishi wa Umma nayo imekuwa ikitumbuiza kwenye sherehe mbalimbali za Serikali na hasa wakati wa utawala wa Awamu ya Tano wa Rais John Magufuli na waliimba wimbo wa maombelezo baada ya kifo cha kiongozi huyo wa nchi.

Kwaya hiyo ya Utumishi wa Umma imekuwa ikisafiri hadi mikoani kwenye shughuli za Serikali kutoa burudani.

Kwaya ya Bunge mara nyingi imekuwa ikitoa burudani kwenye  shughuli za Bunge ikiwamo kuimba wimbo wa Taifa wa siku ya kwanza ya kuanza vikao vya Bunge na wakati wa kuahirisha vikao vya Bunge.

Hata hivyo, kuna kwaya nyingine za majeshi kama vile Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Polisi.

Waimbaji wengi wa kwaya walitokea jeshini akiwamo Kapteni John Komba (marehemu).

Komba alitoka jeshini na kuingia CCM alikoanzisha kwaya ya Tanzania One Theatre (T.O.T) ambayo kazi yake ilikuwa ni kutumbuiza kwenye shughuli za chama hicho cha CCM na ipo hadi sasa.