Samia atoa ahadi ya ujasiri kumuenzi hayati Magufuli
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza ahadi yake ya kutekeleza miradi yote ya maendeleo iliyoasisiwa na Hayati John Magufuli ili kuenzi juhudi za mtangulizi wake huyo.
Chato/Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza ahadi yake ya kutekeleza miradi yote ya maendeleo iliyoasisiwa na Hayati John Magufuli ili kuenzi juhudi za mtangulizi wake huyo.
Akizungumza jana mjini Chato wakati wa kumbukizi ya mwaka mmoja ya kifo cha Dk Magufuli, Rais Samia aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Chato utakaogharimu zaidi ya Sh58.9 bilioni ambao utekelezaji wake umefika asilimia 95 hivi sasa.
Miradi mingine ya maendeleo wilayani Chato iliyoasisiwa na Hayati Magufuli ambayo Rais Samia ameahidi kuikamilisha na kuifungua yeye mwenyewe itakapokamilika ni ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi kitakachogharimu zaidi ya Sh13.2 bilioni na hospitali ya rufaa ya kanda inayojengwa kwa Sh34 bilioni.
“Nawahakikishieni wana Chato kuwa nitatekeleza miradi yote hata ambayo sijaitaja kumuenzi mpendwa wetu Hayati Dk John Magufuli,” alisema Rais Samia wakati wa ibada ya kumbukizi iliyofanyika uwanja wa Magufuli mjini Chato.
Alitaja kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa kivuko cha Chato-Nkome kilichogharimu zaidi ya Sh3.1 bilioni kama mfano wa uthabiti wa ahadi zake kuhusu utekelezaji na ukamilishaji wa miradi iliyoasisiwa katika Serikali ya awamu ya tano.
Miradi mingine ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Serikali ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), kufufua na kuimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na maboresho ya huduma za kijamii katia sekta ya maji, umeme, afya na miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
Mkuu huyo wa nchi na amiri jeshi mkuu alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni ukamilishaji kwa vitendo wa ahadi na ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo yeye na Hayati Magufuli walipita nchi nzima kuinadi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Huku akiwageukia viongozi wa dini, Rais Samia aliwasihi kuendelea kuiombea familia ya Hayati Magufuli na Taifa kwa ujumla ili amani, utulivu na mshikamano viendelee kudumu miongoni mwa ndugu na Watanzania kwa ujumla.
Vilevile, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kushiriki kuweka anwani za makazi pamoja na sensa ya Taifa ya watu na makazi huku akiwasihi wazazi na walezi kutowaficha watoto na ndugu wenye ulemavu kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo jumuishi kwa wananchi wote.
Awali, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimtaja Dk Magufuli kama mwalimu wake, huku akieleza mambo mawili aliyojifunza kwa kiongozi huyo kuwa ni kufanya kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu katika kila jambo, ikiwamo mambo magumu kama maradhi.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi aliwataka Watanzania kuendelea kuyaenzi mema yote yaliyoasisiwa, kusimamiwa na kutekelezwa na Hayati Magufuli ukiwamo ujasiri, busara na umahiri wa kutekeleza mambo kwa maslahi ya Taifa.
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Flavian Kasala aliyeongoza misa hiyo ya kumbukizi aliwataka Watanzania kusimamia ukweli na haki kama sehemu ya kumuenzi kiongozi huyo aliyeongoza Taifa kwa miaka mitano na miezi kadhaa.
Kumbukizi hiyo ilihudhuriwa na mamia ya Watanzania kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Geita, akiwamo Spika Tulia Ackson, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, na viongozi wastaafu ambao ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal na mawaziri wakuu wastaafu Joseph Warioba na Mizengo Pinda. Pia alikuwapo Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda na mke wa Rais Benjamin Mkapa, mama Anna Mkapa.
Licha ya kuwepo hali ya mawingu mazito tangu asubuhi, mvua kubwa ilinyesha mara tu baada ya Misa Takatifu kukamilika, hali iliyotafsiriwa na wenyeji kuwa ni baraka kwa maadhimisho ya kumbukizi hiyo ya kwanza ya Hayati Magufuli.
Maoni ya wananchi
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Jawadu Mohamed alisema kiongozi huyo ataendelea kukumbukwa kwa juhudi zake za ujenzi wa uchumi ulioiwezesha Tanzania kuingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati wa chini kabla ya mwaka 2025 uliolengwa.
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Al Hajj Mustapha Rajab alisema Rais Magufuli alikuwa kiongozi aliyesisitiza kumtanguliza Mungu katika kila jambo linalohusu nchi yake, huku akitaja mapambano dhidi ya Uviko-19 kama mfano hai.
Rehema Peter, mkazi wa jijini Arusha alimkumbuka kiongozi huyo kwa kuruhusu wafanyabiashara ndogondogo kufanya shughuli zao kwa uhuru, jambo analosema litaendelea kusalia kuwa kumbukumbu miongoni mwa wamachinga.
“Tunamuomba Rais Samia aangalie suala la wamachinga tena, kwani maeneo mengine tuliyopewa kwa ajili ya kufanyia biashara zetu mengine hayana biashara, tunamuomba sana mama aangalie hili tena,” alisema Rehema ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo jijini humo.
Wakati wamachinga waliachiwa kufanya biashara hadi kwenye maeneo hatarishi na yasiyoruhusiwa kisheria, Serikali sasa hivi imewapanga kwa kuwatengea maeneo maalumu, huku ikianzisha mpango maalumu wa kuwapa mtaji kupitia mikopo nafuu, ikiwemo kuanzisha benki maalumu pamoja na Shirikisho la Wamachinga Tanzania.
Imeandikwa na Peter Saramba, Rehema Matowo, Mainda Mhando, Musa Juma na Janeth Mushi.