Samia awapiga ‘stop’ mawaziri kuajiri maofisa habari binafsi

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri kuwajibika katika kujibu upotoshaji unaojitokeza kuhusu taarifa za Serikali.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka wizara kujibu kauli za upotoshaji zinazotolewa na wanasiasa kuhusu utendaji wa Serikali.

Katika kulitekeleza hilo, amewataka mawaziri kuacha kuajiri maafisa habari binafsi, badala yake wavitumie vitengo vya habari kutoa taarifa za Serikali.

Rais Samia ameyasema hayo leo, Machi 2, 2023 wakati wa hotuba yake katika mkutano wa faragha na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu katika Ukumbi wa Mikutano wa Arusha (AICC).

Agizo lake hilo kwa wizara linatokana na kile alichokitolea mfano kuwa, amewahi kuibuka mwanasiasa aliyeikosoa Serikali kutumia fedha nyingi kutafuta vyanzo vipya vya maji, ilhali kuna visima kadhaa vilishachimbwa.

Amesema wizara inayohusika na hilo, ilipaswa kusimama haraka na kutolea ufafanuzi kuhusu hilo, badala ya kusubiri taarifa za upotoshaji zisambae.
“Nimewahi kuona kiongozi wa kisiasa akiilaumu Serikali inatumia fedha nyingi kutafuta vyanzo vipya vya maji kupeleka kwa wananchi, ilhali kuna visima kadhaa vilichimbwa nyuma na serikali iliviacha.

“Wizara inayohusika na hili, ilipaswa kusimama haraka kujibu kutoa facts (ukweli), fugures (takwimu) na kumueleza kwanini visima hivyo viliachwa na kwamba vimeachwa au havikuachwa,” amesema.

Mkuu huyo wa nchi amefafanua visima vilivyotajwa na mwanasiasa huyo ndiyo vilivyoisaidia Dar es Salaam wakati wa changamoto ya ukame.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka mawaziri kuacha kuajiri maafisa habari binafsi.

“Najua kila Wizara ina kitengo cha habari, vitengo hivi vinatumikaje, vipo tu vimekaa havifanyi kazi lakini bado mawaziri mmeajiri maafisa wenu habari binafsi wa kutoa taarifa zenu na si taarifa za Serikali, sasa hili tukarekebishe” amesema.