Samia: Wagonjwa wa corona Tanzania wapo zaidi ya 100

Samia: Wagonjwa wa corona Tanzania wapo zaidi ya 100

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ina zaidi ya wagonjwa 100 wa Covid-19 na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili idadi hiyo isiongezeke zaidi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ina zaidi ya wagonjwa 100 wa Covid-19 na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili idadi hiyo isiongezeke zaidi.

Ameeleza hayo leo Jumatatu Juni 28, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wahariri wa vyombo vya habari katika mkutano huo wa tathmini ya siku 100 tangu awe kiongozi mkuu wa nchi.

Amesema ugonjwa huo upo Tanzania na kuna wagonjwa  wanaendelea kupata matibabu, wengi wanatibiwa kwa kutumia gesi kutokana na hali zao kuwa mbaya zaidi.

“Nataka niwe mkweli, Tanzania tuna wagonjwa katika hili wimbi la tatu. Mpaka taarifa nilizozipata juzi, nadhani kuna wagonjwa kama 100 na…, kati yao si chini ya 70 wako kwenye matibabu ya gesi, wengine wako kwenye matibabu ya kawaida,” amesema Rais Samia.

Amesema ukiangalia idadi yao si kubwa lakini hawana budi kujikinga ili wasiongezeke na kwamba Serikali imechukua hatua ya kuchanja na chanjo hiyo itakuwa ya hiari kwa watu ambao watapenda kufanya hivyo.

“Watanzania wengine wameshakwenda kuchanja wapo waliokwenda Dubai, Afrika Kusini..., kwa hiyo tukasema chanjo zije ili watu wachanje kwa hiari,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amebainisha kwamba alipoingia madarakani alitamani kulishughulikia jambo hilo kama linavyoshughulikiwa duniani kwa hiyo aliamua kuunda kamati ili kufuatilia na kuishauri Serikali njia na hatua sahihi za kuchukua.

Amebainisha kuwa jumuiya ya kimataifa pia ilikuwa ikimsukuma kuwaruhusu kuingiza chanjo zao hapa nchini kwa ajili yao pekee, hivyo, katika baraza la mawaziri lililokutana siku chache zilizopita, waliruhusu chanjo hizo ziingizwe nchini kwa usimamizi wa wataalamu wao na wa Tanzania.


“Juzi tulikaa kwenye baraza la mawaziri tukakubaliana kwamba twende kama dunia inavyokwenda,” amesema Rais Samia na kuongeza kwamba tayari Tanzania imewasilisha maombi ya kupata chanjo.