Sau yatambulisha viongozi wake wapya

Muktasari:
Mpata anachukua nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Paul Kyara aliyefariki dunia Desemba mwaka jana.
Dar es Salaam. Chama cha Sauti ya Umma (Sau) kimetambulisha safu mpya ya viongozi wake 14 akiwamo mwenyekiti wa Taifa, Bertha Mpata.
Mpata anachukua nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Paul Kyara aliyefariki dunia Desemba mwaka jana.
Hatua hiyo inatokana na uchaguzi wa ndani wa chama hicho uliofanyika Juni 30, mwaka huu kupitia mkutano mkuu wa kitaifa.
Kwa mujibu wa uongozi wa chama hicho, Sau ina wanachama hai wapatao 700,000 huku ikiwa na uwakilishi wa viongozi kila mkoa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa utambulisho huo, katibu mkuu wa chama hicho, Kisena Kisena alimtaja Bertha ni Issa Zonga kuwa ni makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, John Mswanyama (makamu mwenyekiti bara) na Kisena Fred Kisena (katibu mkuu Taifa).
Wengine ni Amour Ally (naibu katibu mkuu Zanzibar), Majaliwa Kyara (mkurugenzi wa fedha na uchumi), Mariamu Khamisi (naibu mkurugenzi wa fedha na uchumi), Awadh Mtani (mkurugenzi wa uenezi na uchaguzi), Aisha Juma (mkurugenzi wa miradi), Popadick Mbonea (mwenyekiti wa vijana Taifa), Amina Athumani (katibu wa vijana Taifa), Suzana Jackson (mwenyekiti wa wanawake Taifa) na Halima Mshana ambaye ni katibu wa wanawake Taifa.
“Mwenyekiti amechaguliwa kutokana na uwezo wake, tunaamini wanawake wanaweza na hatuna budi kuwapatia fursa hiyo ili watoe mchango wao katika siasa, suala la usawa wa kijinsia ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na chama chetu, tunashauri vyama vingine vitoe nafasi kwa viongozi wanawake,” alisema Kisena.
Mbali na tukio hilo, pia, Sau imepokea wanachama wawili Boaz Mwakasoka na Kunje Ngombale, waliotokea Chama cha ACT Wazalendo.