Sekondari ya Mseke Iringa yakabidhiwa bweni, maabara ya kompyuta
Muktasari:
- Mkurugenzi Mtendaji wa Lyra in Africa, Cikay Richards, ameeleza dhamira ya shirika hilo kuchangia maendeleo ya elimu na uchumi.
Dar es Salaam. Katika juhudi za kukuza ubora wa elimu na kuhakikisha watoto wa kike wa vijijini wanapata elimu bora, shirika la Lyra in Africa, limezindua bweni ya wasichana na chumba cha kompyuta vyenye thamani ya Sh845 milioni katika shule ya sekondari ya Mseke, mkoani Iringa.
Shirika hilo lisilo la kiserikali ambalo limejikita katika kuboresha mazingira ya shule za sekondari za umma kwa lengo la kukuza ubora wa elimu, limesema kujenga miundombinu na kugawa vifaa vya Tehama vitakavyosaidia wanafunzi na walimu katika shule hiyo, kunalenga kuwalinda wasichana kutokana na hatari zinazotokana na kutembea umbali mrefu pamoja na hali ngumu ya maisha kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Lyra in Africa, Cikay Richards amesema dhamira ya shirika hilo kushirikiana na jamii pamoja na Serikali ni kuchochea maendeleo ya elimu na uchumi.
"Dhamira yetu inakwenda mbali zaidi ya ujenzi wa miundombinu na kugawa vifaa vya Tehama. Tumejitolea kukabiliana na changamoto za kimfumo zinazowakabili wasichana wadogo katika kupata elimu bora, lakini zaidi kupambana na umaskini ambalo ndio chimbuko kuu la changamoto za elimu,” amesema Richards.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Veronica Kessy amelipongeza shirika hilo na washirika wake ambao ni Softcat, Greensafe na Michael Matthews Foundation kwa kusimamia na kufadhili mpango huo wenye manufaa makubwa kwa jamii nzima.
“Nawashukuru, kujitolea kwenu kunawawezesha wasichana na vijana wetu kupata elimu katika kiwango kinachokubalika," amesema.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mseke, Ernest Sakafu amesema, "Lyra imekuwa chachu ya mabadiliko katika shule yetu. Ujenzi wa bweni na utoaji wa vifaa vya Tehama utainua uwezo wa kielimu kwa wanafunzi wetu, hasa watoto wa kike ambao wamekuwa wanapata changamoto ya kutembea umbali mrefu.”
Debora Damas Kasela, Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Mseke, ameunga mkono maoni hayo, akisisitiza mchango mkubwa wa Lyra katika maisha ya wanafunzi.
"Hatutapitia tena ugumu wa kulala kwenye sakafu ya darasa, Lyra imetupa hadhi mpya ya utu wetu na imeamsha uwezo wetu wa kunufaika na elimu," amesema Debora.