Selasini amvaa Mbatia, CCM

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumapili Mei 22, 2022, kuhusu vurugu zilizotokeakatika makao makuu ya chama hicho , kulia ni Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini, Mohamedi Tibanyendera. PICHA NA MICHAEL MATEMANGA

Muktasari:

Unaweza kusema miaka 22 ya James Mbatia akiwa mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi inaelekea ukingoni, licha ya kujaribu kuendelea kukalia kiti hicho.

  

Dar es Salaam. Unaweza kusema miaka 22 ya James Mbatia akiwa mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi inaelekea ukingoni, licha ya kujaribu kuendelea kukalia kiti hicho.

Hatua hiyo inatokana na kile kinachoendelea ndani ya chama hicho na tayari Mbatia na baadhi ya vigogo wanaomuunga mkono wamesimamishwa, huku Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikibariki uamuzi huo uliofanywa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Juzi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Joseph Selasini aliyehusika kusimamishwa kwa Mbatia, ameibuka tena na kumtuhumu kiongozi huyo akidai ana ushirikiano wa karibu na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mbatia, ambaye ni mmoja wa waasisi wa chama hicho, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi mwaka 2000, akiwa ametumikia nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (1992 – 1994) na Katibu wa Idara ya Organaizesheni na uchaguzi (1994 – 2000).

Katika kipindi hicho, wachambuzi wanasema Mbatia alifanikiwa kujiimarisha binafsi, lakini alishindwa kukuza chama kwa kuongeza wanachama, kushinda chaguzi sambamba na kukuza vipaji vya wanachama wenye ushawishi.

Tamko la Naibu Msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza alilotoa juzi Mei 25 la kumzuia Mbatia na Sekretarieti yake yote kujihusisha na siasa ndani ya chama hicho, linadidimiza juhudi hizo.

Mei 21, Mbatia pamoja na makamu wake (Bara), Angelina Mtahiwa walisimamishwa na halmashauri kuu ya NCCR Mageuzi kujihusha na shughuli zozote za chama hadi watakapoitwa kwenye mkutano mkuu kujieleza juu ya tuhuma zinazowakabili. Uamuzi huo wa halmashauri kuu ya chama hicho ulioridhiwa na Ofisi ya Vyama vya Siasa ndiyo jaribio kubwa lililotikisa uongozi wa Mbatia katika kipindi hicho, huku akiandamwa na tuhuma kadhaa.

Pia, uamuzi huo unaelezwa na wachambuzi wa siasa, akiwamo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie kuwa ni sehemu ya mapito ya kisiasa yenye mafanikio na changamoto.

“Ameshiriki katika hatua mbalimbali za kuboresha demokrasia ya Tanzania, kwa hiyo hatuwezi kubeza mchango wake katika siasa za Tanzania,” alisema Dk Loisulie.


Mapito ya Mbatia

Katika uongozi wake, chama kimepanda na kushuka katika siasa za Tanzania huku wanachama wake wakimnyooshea kidole pale chama kiliposhuka, hasa katika upotevu wa mali za chama kama vile viwanja na nyumba.

Mbatia alikiwezesha chama hicho kuwa na uwakilishi bungeni kwa NCCR Mageuzi kuvuna wabunge wanne katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, jambo lililokuwa ni mafanikio kwa chama hicho ambacho kilikuwa kimeanza kupoteza mvuto kwa wananchi.

Wabunge waliochaguliwa katika uchaguzi huo kutoka Mkoa wa Kigoma ni Felix Mkosamali (Muhambwe), David Kafulila (Uvinza), Moses Machali (Kasulu Mjini) na Zeitun Buyogela (Kasulu Vijijini).

Mwaka 2011 baada ya Uchaguzi Mkuu, Mbatia alifanya ziara Kigoma kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kukiamini chama hicho na kuwachagua wagombea wa NCCR -Mageuzi kutinga bungeni.

“Mbatia ndiyo amekifanya chama kiendelee kuwepo hadi leo, asingekuwa pale sidhani kama tungekuwa tunakizungumzia chama. Nadhani anafanyiwa fitina tu,” alisema mwanachama wa NCCR-Mageuzi, Deus Msoma, mkazi wa Ilala.

Mafanikio mengine ni Mbatia mwenyewe kuteuliwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kuwa mbunge, mwaka 2012.

Kuteuliwa kwake kulionyesha imani ya Rais kwa Mbatia na chama chake katika siasa nchini.

Kama haitoshi, Mbatia alifanikiwa kuchaguliwa tena kuwa mbunge wa Vunjo katika uchaguzi uliofuata mwaka 2015. Wakati huo alikuwa mbunge pekee aliyewakilisha chama chake bungeni.

Mbatia aliendelea kujiimarisha ndani ya chama kwa kuaminiwa na wanachama wake walioendelea kumchagua kuwa mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi. Mara ya mwisho alichaguliwa Julai 27, 2019 kuongoza kipindi kingine cha miaka mitano ambacho kitakwisha Julai 2024.


Mapinduzi

Kikulacho kinguoni mwako, ndivyo wanavyosema Waswahili, kwa kuwa Selasini aliyekuwa miongoni mwa wanachama wa awali wa NCCR-Mageuzi kabla ya kukimbilia Chadema mwaka 2009 na baadaye kurudi 2020 na kupokewa na Mbatia, ndiye aliyetangaza kumng’oa Mbatia Mei 21, mwaka huu.

“Halmashauri Kuu imeazimia kumsimamisha mwenyekiti Mbatia na makamu mwenyekiti bara hadi pale mkutano mkuu utakapoitishwa mapema mwaka huu na kuja kujieleza,” alisema Selasini ambaye amejitambulisha ni mjumbe wa halmashauri kuu.

Septemba 22, 2015, chama hicho kilimsimamisha uongozi makamu mwenyekiti wa chama hicho, Leticia Mosore kwa madai ya kukihujumu. Hata hivyo, Msajili wa Vyama, Jaji Mutungi alimrejesha.

Mbatia pamoja na bodi ya wadhamini wamekuwa wakinyooshewa kidole katika usimamizi wa mali za chama na kikao cha halmashauri kuu kiliamua kuivunja bodi ya wadhamini na kuteua wajumbe wapya wa bodi hiyo.

Akizungumza na wanahabari jana jijini hapa, Selasini alikanusha kutumia wajumbe feki kumng’oa Mbatia, akidai kulikuwa na wajumbe halali 52 kati ya 82 waliotakiwa kuwepo.

“Hakuna suala la wajumbe feki, wote walirekodiwa na kuwekwa kumbukumbu zao, maneno kwamba tumempindua Mbatia ni ya uongo,” alidai Selasini.

Alidai licha ya Mbatia kutokuwepo kwenye mkutano huo Makamu Mwenyekiti Zanzibar alikuwepo na kikao kikaendelea.

“Halmashauri Kuu haina mamlaka ya kumfukuza Mwenyekiti, ilichofanya ni kumsimamisha hadi pale mkutano mkuu utakapofanyika,” alisema Selasini. Akizungumzia tuhuma zinazomkabili Mbatia, alisema ya kwanza ni uhusiano wake na CCM, hivyo Halmashauri Kuu imefikia uamuzi huo na kumtaka kuacha uhusiano huo. Selasini aliitaka CCM kutoitumia NCCR-Mageuzi katika kubatilisha mambo yake na kumshauri Mbatia kuheshimu vikao halali vya chama, ikiwamo Halmashauri Kuu iliyokutana Mei 21.

Jana Mbatia hakupatikana kuzungumzia madai hayo, baada ya simu yake kuita bila kupokewa.

Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye anayemuunga mkono Mbatia alisema wana uwezo wa kumjibu Selasini, lakini hawana muda wa kujibizana akidai kilichokisema hakina ukweli.

“James (Mbatia) ana mambo mengi ya kufanya, hawezi kujibu uongo kama ule aliousema Selasini,” alisema Simbeye.


Wasomi wafunguka

Akichambua zaidi miaka 22 ya Mbatia kama mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Loisulie alisema kwa uongozi wake chama hicho kimekuwa kikishuka mwaka hadi mwaka.

Pia, alisema Mbatia hakufanikiwa kuwaandaa watu wenye nguvu ya ushawishi kwenye chama hicho, jambo linaloonyesha kwamba hakina watu wengine wenye ushawishi zaidi yake.

“Katika eneo hilo, Mbatia hakufanya vizuri katika kujenga watu, kukuza vipaji ndani ya chama ndiyo maana ukimwondoa yeye, sidhani kama kuna mtu mwingine ambaye amejijenga kiasi kwamba anaweza akasikilizwa kama yeye,” alisema.

Maoni hayo yameungwa mkono na mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza aliyesema miaka 22 ya uongozi wa Mbatia imeirudisha nyuma NCCR-Mageuzi kwa sababu wakati inaanzishwa, ilikuwa chama kikuu cha upinzani na katika uchaguzi wa mwaka 1995 ilipata viti 27 bungeni.

“Mwaka 2000 baada ya kuingia Mbatia, chama hicho kimekuwa kikirudi nyuma…chama hakijaenea kwa wananchi, shughuli za chama hazionekani kwenye vyombo vya habari, ukiona NCCR basi ni mwenyekiti ana-react jambo fulani lakini siyo wanachama,” alisema.

Nyongeza na Fortune Francis na Bakari Kiango.