Serikali: Changamoto za vijana ni zaidi ya fedha
Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka.
Muktasari:
- Waziri Joel Nanauka amesema baadhi ya vijana wanashindwa kurejesha mikopo na kukosa sifa za msingi, hivyo Serikali inapanga kusajili kampuni 20,000 kufikia 2030 ili kuongeza ushiriki kwenye zabuni za umma. Viongozi wengine wamehimiza uzalendo, amani na kuepuka vurugu, wakisisitiza maendeleo ya vijana yanahitaji mfumo mpana wa uwezeshaji.
Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu changamoto za vijana nchini ukiendelea kutawaliwa na hoja ya ukosefu wa mitaji na ajira, Serikali imesema matatizo yanayolikabili kundi hilo ni zaidi ya fedha.
Imesema si kwamba vijana hawapatiwi fedha, baadhi yao wamekopeshwa lakini wameshindwa kulipa, wengine wanakosa sifa za msingi, ikiwemo vitambulisho vya Taifa, huku wakiendelea kulalamika.
Hayo yameelezwa leo, Jumamosi, Mei 16, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, alipozungumza katika Kongamano la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu lililofanyika jijini Dar es Salaam lenye kaulimbiu ya ‘Never Again’.
Amesema licha ya Serikali kuweka mazingira ya kuwawezesha vijana kiuchumi, bado sehemu kubwa ya kundi hilo halijajiandaa kutumia ipasavyo fursa zilizopo.
“Tatizo la vijana ni zaidi ya fedha, ndiyo maana sera ya vijana haizungumzi kitu kimoja, inagusa mambo mbalimbali yatakayomfanya huyu kijana kuwa kijana aliyekamilika,” amesema.
Amesema hata katika mikopo inayotolewa kwa vijana, changamoto bado ni kubwa, kwani baadhi yao wanashindwa kurejesha, hali inayodhoofisha mzunguko wa uwezeshaji kwa wengine.
“Katika wizara yetu kuna Sh3.9 bilioni zilizokopeshwa vijana ambazo bado hazijarejeshwa. Hii inaonesha changamoto si fedha pekee, bali namna ya kujiandaa kuzitumia fursa hizo,” amesema.
Nanauka amesema Serikali imepanga kufikia mwaka 2030 kusajili vikundi na kampuni 20,000 za vijana ili zishiriki kikamilifu katika zabuni za Serikali kupitia mfumo wa manunuzi ya umma.
Kwa mujibu wa waziri huyo, Sheria ya Manunuzi ya Umma inazitaka taasisi za Serikali kutenga asilimia 30 ya manunuzi kwa makundi maalumu yakiwemo wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.
Amesema ndani ya asilimia hiyo, vijana wanatakiwa kupata asilimia 10, kiwango ambacho kwa mwaka wa fedha uliopita kilikuwa sawa na takribani Sh3 trilioni.
“Tatizo lililopo ni kwamba vijana wengi hawana kampuni zilizosajiliwa wala uwezo wa kufuatilia zabuni. Ndiyo maana Serikali sasa inataka kuhakikisha wanasajiliwa ili waweze kunufaika,” amesema.
Uimara wa Tanzania
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema Tanzania imeendelea kuwa imara kutokana na uzalendo wa wananchi wake licha ya kupitia vipindi mbalimbali vya misukosuko.
“Nchi hii imepita mapito mengi, lakini imeendelea kubaki imara kutokana na uzalendo wetu na upendo wa wananchi kwa Taifa lao,” amesema.
Kabudi amesema baadhi ya matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 hayakuwa ya kawaida na hayakupaswa kupewa nafasi ya kujirudia.
“Kaulimbiu ya Never Again ina maana kuna jambo lililotokea si la kawaida na limetutikisa kama Taifa. Ni lazima tukubaliane kwamba yasitokee tena,” amesema.
Amewataka vijana kutambua kuwa Tanzania ndiyo nchi yao pekee na kwamba kuharibu amani ya Taifa ni kuhatarisha mustakabali wao wenyewe.
“Ukiiharibu Tanzania hakuna Tanzania nyingine. Msidhani kuna nchi itakayowapokea kwa mikono miwili mkiivuruga nchi yenu,” amesema.
Hatari ya vurugu
Kiongozi wa CCM Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje, naye ameonya juu ya athari za vurugu kwa uchumi wa nchi na ajira za vijana.
Wenje, ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Chadema Kanda ya Victoria, amesema watu wengi wanafikiri kuchoma mali au kufanya vurugu ni kuidhuru Serikali pekee, bila kuelewa madhara yake kwa wananchi wa kawaida.
“Ukichoma kituo cha mafuta umeharibu mnyororo mzima wa ajira. Kuna wafanyakazi, madereva, wafanyabiashara na familia zinazotegemea shughuli hizo,” amesema.
Ametolea mfano maandamano ya Gen-Z nchini Kenya yaliyosababisha hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na kusimama kwa shughuli za kiuchumi.
“Nchi ikichomwa tutabaki na nini? Ukienda hata Rwanda utaitwa mkimbizi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Wenje amesema vijana wengi wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya ushawishi wa mitandao ya kijamii na wanasiasa wanaotumia umaarufu kupotosha umma.
Amesema baadhi ya viongozi wa kisiasa hujenga ushawishi mkubwa kwa kutumia hisia za watu bila kuwaeleza athari za matendo wanayowasukuma kuyafanya.
“Kumpa nchi mwanasiasa anayetafuta umaarufu ni sawa na kumpa mtoto msumeno; atakata kila kitu bila kujua madhara yake,” amesema.
Pia, amesisitiza umuhimu wa maridhiano katika siasa, akisema viongozi wanaokataa mazungumzo hawaijengei nchi mazingira ya utulivu.
“Kiongozi anayekataa maridhiano hapendi Taifa kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Uwezeshaji vijana
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amesema changamoto za vijana wengi wa sekta isiyo rasmi pia zinachangiwa na mifumo kandamizi ya kiuchumi inayowafanya kufanya kazi katika mazingira magumu.
Amesema amepiga marufuku mikataba ya kinyonyaji kwa madereva wa bodaboda baada ya kubainika kuwa baadhi yao hulazimika kurejesha zaidi ya mara mbili ya thamani ya pikipiki wanazoendesha.
“Unakuta bodaboda ya Sh3 milioni kijana anatakiwa kurejesha Sh6 milioni. Hali hii ndiyo inayowasukuma kuendesha kwa mwendokasi ili wawahi kupeleka hesabu ya kila siku,” amesema.
Amesema vijana wengi wanahitaji kurasimishwa kwa kupata vyeti vya kuzaliwa na nyaraka nyingine ili waingie katika mifumo rasmi ya mikopo na uwezeshaji.
Katika kongamano hilo, viongozi walikubaliana kuwa changamoto za vijana haziwezi kutatuliwa kwa fedha pekee, bali zinahitaji mchanganyiko wa elimu, uzalendo, maadili, uwekezaji katika ujuzi na mazingira rafiki ya kiuchumi.