Serikali kuja na mkakati mpya wa elimu kuondoa changamoto ya ajira
Muktasari:
- Mfumo mpya unaotokana na sera ya elimu na mtalaa mpya utawezesha kumsogeza mhitimu kujiajiri au kuajiriwa kwa kumpa utaalamu akiwa shuleni kwa miaka 10.
Dodoma. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mfumo mpya wa elimu utakaokuwa na mikondo miwili, utakaoanza mwaka 2027, utamwezesha mhitimu kupata utaalamu akiwa shuleni kwa miaka 10 na hivyo kuajirika kirahisi.
Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Novemba 8, 2024 wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2025/26 na Mapendekezo Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2025/26.
Amesema mfumo wa elimu wa sasa ambao elimu ya lazima ni darasa la saba, unamfanya mwanafunzi anayemaliza elimu hiyo kukosa vigezo vya kujiari na kuajirika kutokana na kuwa na umri mdogo.
Profesa Mkenda amesema mfumo mpya ambao unatokana na sera ya elimu na mitalaa mpya utawezesha kumsogeza mhitimu kujiajiri au kuajiriwa kwa kuwa utamwezesha kuwa shuleni kwa miaka 10.
Amefafanua kuwa mfumo huo mpya unaanzia elimu ya awali kwa mwaka mmoja, elimu ya msingi miaka sita, elimu ya chini ya sekondari miaka minne, elimu ya juu ya sekondari miwili au mitatu na baada yake elimu ya juu.
“Elimu ya lazima sasa itakuwa ni miaka 10 sio miaka saba tena, maana yake mtoto atakapoanza darasa la kwanza ni hadi darasa la sita na atalazimika kukaa shuleni hadi amalize kidato cha nne,” amesema.
Amesema mtoto atakapoanza shule katika mfumo huo mpya, atamaliza masomo ya kidato cha nne akiwa na miaka sita, ambapo watakuwa wamemsogeza na umri unaokubalika kujiajiri au kuajiriwa.
Amesema nchi nyingi duniani zinakimbilia umri wa lazima shuleni kuwa miaka tisa hadi 12 na kutolea mfano wa Zanzibar ambako ni miaka tisa na Kenya ikiwa ni miaka 10.
Amesema mfumo huo utaanza kwa watoto ambao wako darasa la tatu ambao walianza na mtaala mpya na kuwa itakapofika mwaka 2027 ni lazima wote watakaomaliza darasa la sita wataendelea na masomo ya sekondari.
Amesema ndiyo maana uwekezaji katika shule, miundombinu kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ni mkubwa na utaongezeka ili kuwezesha kila eneo kuwa na shule ambazo mwanafunzi anaweza kufika na kusoma.
Aidha, Profesa Mkenda amesema katika mfumo huo mpya, somo la Kiingereza litaanzia darasa la kwanza na litafundishwa kimawasiliano zaidi, halafu baadaye kikanuni.
Amesema katika chaguo la sasa kuna uwezekano wa mwanafunzi kuongeza lugha nyingine zaidi ya mbili, ambapo watajitahidi wawepo walimu wa lugha mbalimbali katika shule hizo.
Pia amesema wanafunzi wataweza kujifunza ukalimani ili kuwawezesha wanaomaliza kwenda sehemu yoyote duniani kutafuta ajira.
Amesema baada ya mwanafunzi kumaliza shule ya msingi, inagawanyika mikondo miwili ya elimu jumla na amali (ni kama mafunzo ya ufundi na ufundi stadi).
“Tunavyoongea, sasa hivi tayari tumeanza ujenzi wa shule 100 za ziada, za ufundi, Tanzania sio amali, ni amali ufundi na tumepeleka kwa wabunge ambao Veta (chuo cha Elimu na Ufundi Stadi) inajengwa kwa mbunge mwenzake,” amesema.
Amesema baada ya kumaliza kidato cha nne, wahitimu hao watakuwa na cheti cha kidato cha nne na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) ambapo wataweza kufanya kazi mbalimbali baada ya kumaliza masomo yao.
Amesema kwa wanafunzi watakaofuata mkondo wa amali- ufundi, wakaenda masomo ya kidato cha tano na sita watatoka na cheti cha kidato cha sita na NACTVET na hivyo wanaweza kwenda kujiajiri au kuajiriwa.