Serikali kushirikiana na wadau kupunguza uhaba watumishi sekta ya afya

Mkurugenzi wa Miradi Mkapa Foundation, Rachel Sheiza akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Kisayansi wa Huduma za Afya ya Uzazi,Mtoto,Vijana na Lishe

Muktasari:

  • Serikali imesema itaendelea kushirikisha na sekta binafsi kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi katika sekta ya afya ili kukabiliana na tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi hapa nchini.


Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kushirikisha na sekta binafsi kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi katika sekta ya afya ili kukabiliana na tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi hapa nchini.

Imeelezwa kuwa takribani asilimia 90 ya vifo vitokanavyo na uzazi vinatokea katika vituo vya afya kutokana na kukosekana kwa wataalamu, huku asilimia 10 vikitokea majumbani.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya kutoka Tamisemi, Dk Ntuli Kapologwe amezungumza hayo leo Alhamisi Novemba 11, 2021 katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika watumishi kwa lengo la kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto wakati wa Mkutano wa mwaka wa kisayansi wa huduma za afya ya uzazi, mtoto, vijana na lishe.

Akielezea jinsi Serikali kupitia Tamisemi inavyosimamia utoaji huduma za afya katika mikoa na halmashauri, Dk Kapologwe amesema Serikali bado inakabiliwa na uhaba wa watumishi katika sekta ya afya jambo ambalo linahitaji ushirikishwaji wa sekta binafisi ili kuendelea kuimarisha utoaji huduma.

“Bado tuna tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi. Ukiangalia takwimu ni kwamba takribani asilimia 90 ya vifo vinavyotokana na uzazi vinatokea katika vituo vyetu vya kutolea huduma kwa sababu ya uhaba wa watumishi na pia waliopo baadhi yao hawana umahili na ujuzi wa kukabiliana na matatizo haya,” amesema Dk Ntuli.

Akieleza mipango ya Serikali kukabiliana na tatizo hilo, Dk Ntuli amesema tayari Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Tamisemi na wadau walizindua mwongozo wa kitaifa wa kujitolea (National Health Workforce Volunteerism Guideline) kama sehemu ya mkakati mahususi wa kuboresha huduma za afya kwa kukabiliana na uhaba wa watumishi katika sekta hiyo.

“Pamoja na mwongozo huu ambao tutaendelea kuutekeleza hivi karibuni, tunawashukuru wadau kutoka sekta binafsi kama vile Mkapa Foundation, MDH, Amref na wengine ambao wamekuwa wakiwekeza katika eneo hili kwa kuajiri watumishi wa afya kwa miongozo ya serikali na kuwapeleka katika vituo vya Serikali katika halmashauri zetu,” Ameongeza Dk Ntuli.

Awali akitoa uzoefu wa utekelezaji wa afua za upatikanaji wa watumishi wa afya kupitia sekta binafsi, Mkurugenzi wa Miradi kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Rahel Sheiza amesema kulingana na takwimu zilizopo wadau kutoka sekta binafsi (NSAs) wanachangia zaidi ya ajira 3,000 za watumishi kila mwaka katika sekta ya afya wanaochangia utoaji wa huduma bora za mama, mtoto, baba na vijana.

Pamoja na jitihada hizo kutoka kwa wadau,  bado mchango huo wa watumishi wanao ajiriwa na wadau mbali mbali katika sekta ya afya hauakisiwi katika taarifa za idadi ya watumishi nchini, hivyo ni dhahiri kuwa pengo lililopo hivi sasa la asilimia 52 linaweza kuwa chini zaidi kama mchango wa wadau utajumuishwa katika taarifa za watumishi.

“Ukosefu wa takwimu hizi hususani katika kuanisha upungufu wa watumishi wanaohitajika na waliopo kwenye sekta ya afya hapa nchini unasababisha pia kutokuwa na mipango thabiti katika nchi. Kwa mfano Mkapa Foundation pekee tumeajiri watumishi 1263 katika Halmashauri 161  wanaotoa huduma za Afya ya Mama na Mtoto katika ngazi zote za vituo vya huduma za Afya. Hawa wakiingizwa katika takwimu za kitaifa upungufu huo unaweza kuwa chini kidogo,” amesema Sheiza.

Akizungumzia kuhusu mwongozo wa Kitaifa wa Kujitolea (National Health Workforce Volunteerism Guideline), Sheiza amesema Taasisi ya Mkapa Foundation inaamini kuwa utekelezaji wa mpango huu katika ngazi za vituo vya huduma za Afya ni moja kati ya njia itakayo saidia kupunguza changamoto ya watumishi katika vituo vya huduma za afya kabla ya ajira rasmi kutolewa na Serikali.

“Sisi Mkapa Foundation tumeshiriki katika kila hatua wakati wote wa kuandaa mwongozo huu mpaka unazindulia, endapo serikali kupitia watausimamia utekelezwe kama unavyokusudia, utaleta matokeo chanya hususani katika utoaji huduma za Afya ya Mama na Mtoto kwa kuwa watumishi wakutosha watakuwepo katika vituo vya kutolea huduma,” ameongeza Sheiza.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru,  Dk Maneno Focus akichangia  mdahalo huo, amesema ipo haja ya serikali kuja na mkakati maalumu wa utekelezaji wa mwongozo huo ili kila Halmashauri zote ziweze kunufaika na uwepo wake.

“Tunahitaji mpango harakishi utakaotuwezesha tuanze kutumia watumishi wa kujitolea ili tuendelee kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Hawa watumishi wapo, ni swala la kujipanga hususani kupitia mapato ya ndani ili tuweze kuimarisha utoaji huduma. Amesema Dk Focus.