Serikali kutoa ratiba mabasi kusafiri saa 24

Muktasari:

Serikali imerejesha utaratibu wa mabasi ya mikoani kusafiri saa 24 kuanzia Oktoba 1 mwaka huu baada ya kujiridhisha juu ya uwezo wa polisi kudhibiti usalama katika maeneo mbalimbali.

Dar es Salaam. Serikali imetangaza rasmi kutoa ratiba kamili ya mabasi ya mikoani kusafiri saa 24 kuanzia Oktoba 1 mwaka huu baada ya kujiridhisha juu ya uwezo wa polisi kudhibiti usalama katika maeneo mbalimbali.

Hatua hiyo ya Serikali inakuja baada ya kuonekana uhitaji wa watu mbalimbali kutaka kusafiri usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kufanya tathmini na kujiridhisha kuwa udhibiti kupitia Jeshi la Polisi umeimarika.

"Serikali inatangaza rasmi kuanza kutoa ratiba rasmi ya mabasi kusafiri kwa saa 24 kuanzia Oktoba 1 mwaka 2023,"amesema Sagini.

Pia kuongezeka kwa mwamko wa wananchi haswa wafanyabiashara kutumia taasisi za kifedha na kuacha tabia ya kutembea na fedha taslimu (cash).

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani, Ramadhani Ng'anzi amesema kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha linaimarisha usalama ili raia na mali zao kuwa salama wanapokuwa safarini.

Ng'azi pia alitoa wito kwa madereva kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni za usalama barabarani

Nae Mkurugenzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Johansen Kahatano amesema kabla ya kutoa ratiba kwa wasafirishaji watatakiwa kusaini tamko ambalo litakuwa na mambo mahususi ya kuzingatia.

Alibainisha mambo hayo kuwa ni pamoja na madereva kutakiwa kuwa wamesajiliwa katika mfumo wa Latra, kuwa na mtu maalum ambaye atafatilia mabasi hayo nyakati za usiku, taarifa za abiria kuingizwa kwa usahihi katika mfumo wa tiketi mtandao.

Nae, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Priscus Joseph akizungumza na kituo cha runinga cha Azam Tv, amesema uamuzi huo utawasaidia wananchi kuachana na tabia ya kupanda usafiri usio rasmi nyakati za usiku.