Serikali kuwalipa posho madiwani, maofisa tarafa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 posho za kila mwezi za madiwani zitalipwa Serikali kuu.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 posho za kila mwezi za madiwani zitalipwa Serikali kuu.

Ameeleza hayo leo Alhamisi Juni 10, 2021 wakati akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bungeni mjini Dodoma.

Amesema fedha hizo zitaingizwa  moja kwa moja kwenye akaunti zao kwa halmashauri zote zenye uwezo mdogo kimapato huku halmashauri 16 zenye uwezo mkubwa wa kimapato zitaendelea kutumia mapato yake ya ndani kulipa posho za madiwani kupitia kwenye akaunti zao.

“Madiwani wenzetu wanafanya kazi nzuri sana za kusimamia shughuli za maendeleo kwenye kata zetu. Hawa ni wabunge wakaazi wa kwenye kata zetu ambao kila siku wako na wananchi wetu kwenye kusimamia shughuli za maendeleo.”

“Napenda niwaeleze kuwa mama yetu amesikia kilio chenu na alinielekeza mimi pamoja na Waziri wa Tamisemi kulitafutia ufumbuzi suala hili,” amesema.

Kuhusu maofisa tarafa amesema kuanzia mwaka 2021/22, Serikali Kuu ianze kulipa posho ya  Sh100,000 kwa mwezi kwa kila ofisa tarafa ili waweze kumudu gharama za mafuta na matengenezo ya pikipiki.

Pia, watendaji kata kuanzia mwaka 2021/22, Serikali

Itaanza kulipa posho ya Sh100,000 kwa mwezi kwa kila mtendaji kata kupitia mapato ya ndani ya halmashauri yaliyokuwa yakitumika kulipa madiwani.