Serikali ya Tanzania yaitangaza Wilaya ya Chato kitovu cha uhifadhi na utalii Kanda ya Ziwa

New Content Item (1)
Serikali ya Tanzania yaitangaza Wilaya ya Chato kitovu cha uhifadhi na utalii Kanda ya Ziwa

Muktasari:

Chato imechaguliwa kuwa kitovu cha utalii kutokana na eneo lake kuwa na sifa ya kuwa na utalii wa fukwe, utalii wa majini na ule wa nchi kavu ambapo mtalii anaweza kuona wanyama ,kupiga picha na kuwinda.


Geita. Serikali ya Tanzania imeitangaza Wilaya ya Chato mkoani Geita kuwa kitovu cha uhifadhi na utalii wa Kanda ya Ziwa.

Hayo yameelezwa jana jioni Jumanne Januari 12, 2021 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alipotembelea shamba la miti Biharamulo lililopo wilayani humo.

Ndumbaro amesema Chato imechaguliwa kuwa kitovu cha utalii kutokana na eneo lake kuwa na sifa ya kuwa na utalii wa fukwe, utalii wa majini na ule wa nchi kavu ambapo mtalii anaweza kuona wanyama ,kupiga picha na kuwinda.

Amebainisha kuwa Serikali imelenga kuunganisha utalii kutoka hifadhi ya Serengeti hadi Chato kupitia visiwa vya Saanane hadi Rubondo na baadaye mtalii anaweza kutembelea hifadhi ya Burigi Chato.

Ndumbaro amewataka wawekezaji katika sekta ya utalii kuanza kuwekeza kwenye utalii wa maji ili kuvutia watalii watakaofika maeneo hayo.

Amesema wizara imejipanga kutangaza utalii wa Kanda ya Magharibi na kanda ya ziwa ili uweze kutambulika kama inavyotambulika Kanda ya Kaskazini ambayo kitovu chake cha uhifadhi ni Mkoa wa Arusha.

Amefafanua kuwa katika kutangaza vivutio vilivyopo katika eneo la Kanda ya Ziwa, Serikali imelenga kuwa na mkutano mkubwa wa wadau wa utalii wa kanda hiyo ili wajue vivutio vilivyopo waweze kuvitangaza.