Serikali yachunguza watumishi wa afya kumwagiana ‘dripu’

Muktasari:

  • Saa chache baada ya video inayoonyesha wahudumu wa afya katika kituo cha afya Nyankumbu wakisherehekea siku ya kuzaliwa kwa kumwagiana majitiba ‘dripu’ kuanza kusambaa mitandaoni, Wizara ya Afya imesema tayari imeanza kufanya uchunguzi wa sakata hilo.

Dar es Salaam. Serikali iemanza kufanya uchunguzi kuhusu video inayosambaa mtandoni ikiwaonyesha watoa huduma za afya wakisherehekea siku ya kuzaliwa kwa kumwagiana majitiba maarufu ‘dripu’.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Desemba 3, 2023 Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amesema bado video hizo hazina uhalisia na eneo linalotajwa, hivyo wanashirikiana na waganga wakuu wa maeneo husika kujiridhisha.

“Nimeiona asubuhi hii tunafuatilia, inaonekana kama hicho kituo kilichoandikwa pengine si chenyewe, lakini hatujapata uhakika vizuri,” amesema.

Profesa Nagu amesema wanafuatilia kupitia Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Geita, lakini bado hawana uhahika kama ni kituo  cha Serikali au cha binafsi.

“Tumeona picha za watu, lakini tunafuatilia kuona ni kituo gani, inawezekana pia si jina la kituo kilichoandikwa, tukishafuatilia tutatoa majibu mpaka tupate ukweli wa tukio lenyewe,” amesema Profesa Nagu.

Katika video hiyo iliyokuwa na maelezo kuwa ni watumishi wa afya katika kituo cha afya Nyankumbu, walionekana wanatumia maji ya kutibia wagonjwa (dripu) kwa sherehe yao ya kuzaliwa.

Hata hivyo, maoni ya watu mbalimbali katika mtandao wa kijamii wa Instagram yalijikita kwa Wizara ya Afya kutolea ufafanuzi jambo hilo, wakitaka ichukue hatua na kama kuna uvunjifu wa maadili ya utumishi wa afya, uwajibikaji uwepo.

“Watanzania wanakosa dawa na vifaa tiba huko kwenye vituo vya afya vijijini, lakini wengine wanafanyia birthday?” amehoji Amos James.

“Unatumia mali ya Serikali iliyogharimu mabilioni ambayo kule Tanga mama mjamzito alipoteza uhai kwa kukosa tu pesa ya huduma ya upasuaji, huduma ambayo huenda angeipata bila kulipa chochote,” amesema Abdul Salaam.


Fahamu kuhusu dripu

Mfamasia na Mkufunzi wa Shule ya Famasia wa Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba amesema majitiba yanayotumika kumwekea mgonjwa kupitia mishipa ya damu kawaida nusu lita huuzwa Sh2,000 japokuwa inategemea na ujazo husika kama ni lita moja ni zaidi ya hapo.

Alipoulizwa iwapo kuna madhara yoyote ambayo mtu anaweza kuyapata akitumia ndivyo sivyo, Mnyemba amesema hakuna madhara,  isipokuwa kama mtu atakunywa mengi anaweza kuharisha.

“Ukinywa mengi unaweza kuharisha, lakini kuna mengine hayana madhara yoyote, ukinywa yenye sukari nyingi inapandisha sukari ghafla na kuna mengine yana madini mengi akitumia anaweza kupata madhara.

“Kwa kunywa hayana madhara, lakini hayatakuwa na faida ya moja kwa moja. Majitiba yanatakiwa kutumika kwa kuingiza moja kwa moja kweye mishipa ya damu, kwani hata ukinywa hayakati kiu kirahisi kama maji ya kawaida,” amesema Mnyemba.