Serikali yaendelea kuwasaka waliovujisha mitihani ya utabibu
Muktasari:
Serikali ya Tanzania imesema uchunguzi wa kuwabaini watu, vyuo na taasisi vilivyojihusisha na kuvuja kwa mitihani ya utabibu nchini Tanzania huku Baraza la Ufundi la Taifa (NACTE) likiagiza kurudiwa upya kwa mitihani hiyo ndani ya wiki sita kuanza Novemba Mosi mwaka huu.
Dodoma. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema inaendelea na uchunguzi wa kuwabaini watu, vyuo, taasisi vilivyojihusisha na kuvuja kwa mitihani ya utabibu nchini Tanzania.
Mganga Mkuu wa Serikali Dk Aifello Sichalwe amesema leo Alhamis Novemba 4, 2021 kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
“Wizara imesikitishwa na itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kukamilisha uchunguzi na kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki kufanya udanganyifu kwani vina madhara makubwa kwao na jamii,”amesema.
Amesema mtaalamu wa afya aliyejipatia sifa kwa njia udanganyifu ni hatari kwa afya za wananchi na kuwaomba wananchi waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali kuwa ipo makini na itatumia jitihada zote kulinda usalama.
Aidha, Dk Sichalwe amesema Baraza la Taifa la Ufundi (Nacte) limeagiza kurudiwa kwa mitihani hiyo ya program ya utabibu ngazi ya tano (NTA level 5) ndani ya wiki sita kuanzia Novemba Mosi mwaka huu.
Amesema mitihani hiyo itafanyika sambamba na mitihani ya marudio kwa program nyingine za afya nchi nzima.
Wizara hiyo imewataka wakuu wa vyuo vyote vya afya nchini kuwapa taarifa wanafunzi ili wajiandae kwa ajili ya mitihani yao.
Mwananchi lilikuwa ni gazeti la kwanza kuibua kuvuja kwa mitihani hiyo kupitia mitandao ya jamii katika makundi ya WhatsApp na Telegram.