Serikali yahamasisha matumzi ya bayoteknolojia

Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Toba Nguvila akihutubia mkutano mkuu wa BST leo jijini hapa.
Muktasari:
- Serikali imeandaa Sera mpya ya Taifa ya Mazingira ya 2021 inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa bayoteknolojia ya kisasa inatumika kwa usalama bila kuleta athari hasi kwa afya ya binadamu, wanyama, mazingira na uchumi.
Dar es Salaam. Serikali imesema inatambua manufaa ya matumizi ya bayoteknolojia ya kisasa na ndio maana imeandaa mfumo wa Taifa wa Kusimamia Matumizi Salama wa mwaka 2007 ukijumuisha sera, sheria, kanuni, taratibu na mikakati ya utekelezaji na usimamizi.
Hayo yameelezwa leo Desemba 5, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Toba Nguvila aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano, Mazingira), katika mkutano wa mkuu wa mwaka wa Chama cha Bayoteknolojia Tanzania (BST) jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na hofu ya matumizi ya mazao ya bayoteknolojia kwa madai ya kuathiri afya ya binadamu.
Hata hivyo, Nguvila amesema kwa kutambua umuhimu wake, Serikali iliandaa sera mpya ya Taifa ya Mazingira ya 2021 inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa bayoteknolojia ya kisasa inatumika kwa usalama bila kuleta athari hasi kwa afya ya binadamu, wanyama, mazingira na uchumi.
Amesema sera inalenga “Kuimarisha uwezo wa kitaifa katika kusimamia matumizi salama ya bayoteknolojia ya kisasa na bidhaa zake, kuongeza uelewa wa umma katika kusimamia matumizi salama na endelevu na kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika masuala ya uendelezaji na usalama wa teknolojia hiyo.”
Amezitaja sera nyingine zinazosimamia matumizi salama ya bayoteknolojia kuwa pamoja na Sera ya Taifa ya Bayoteknolojia ya mwaka 2010 inayosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi ma Teknolojia na Sera ya Taifa ya Kilimo chini ya Wizara ya Kilimo.
“Hali kadhalika, Serikali imetunga Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004, ambayo pamoja na mengine ina vifungu vinavyosimamia usalama wa mazingira dhidi ya athari zinazoweza kutokana na bayoteknolojia,”amesema.
Hata hivyo, amesema kwa sasa Serikali inakusanya maoni na mapendekezo ya wadau kwa lengo la kupitia upya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004 ili iweze kukidhi mahitaji ya mbalimbali kwa lengo la kupitia upya sasa.
“Serikali pia inakusanya maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu Kanuni za usimamizi wa matumizi salama ya bayoteknolojia ya kisasa ya mwaka 2009, kama zilivyofanyiwa marekenisho mwaka 2015,” amesema.
Akizungumzia hofu ya wananchi kuhusu matumizi ya bayoteknolojia, Nguvila amesema kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia duniani, Tanzania haiwezi kukwepa matumizi ya bayoteknolojia kukuza uchumi.
“Bado wako baadhi ya watu ambao wana mashaka au wanapinga matumizi ya teknolojia hii hususani sekta ya kilimo. Hali inasababishwa kwa kiasi kikubwa na uelewa mdogo wa dhana ya teknolojia hii hata miongoni mwa wanasiasa, watendaji wa serikali, wataalamu na jamii kwa ujumla,” amesema.
Awali, akimkaribisha kiongozi huyo, Mwenyekiti wa BST, Profesa Peter Msola amesema matumizi ya bayoteknolojia yameshika kasi duniani kote kwa kutambua manufaa yake katika kilimo, afya, mifugo, viwanda, mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
“Hapa nchini tumeshuhudia ongezeko la bidhaa zitokanazo na bayoteknolojia kama viuatilifu, vyakula, mazao ya mifugo, mbinu za kubadilisha taka za viwandani kuwa mbolea, viuatilifu vya kibaiolojia vya kuua viluwiluwi vya mbu na wadudu waharibifu shambani,” amesema.
Hata hivyo, amesema bado kuna uelewa mdogo kwa baadhi ya wadau kuhusu matumizi ya bayoteknolojia ya kisasa na nchi kushindwa kupiga hatua katika utafiti na matumizi yake katika sekta ya kilimo.