Serikali yaipa NFRA Sh15 bilioni za kununua mahindi

What you need to know:

  • Serikali imewapa Sh15 bilioni Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili waweze kununua mahindi ya wakulima.



Dodoma. Serikali imewapa Sh15 bilioni Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili waweze kununua mahindi ya wakulima.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Septemba 2, 2021 na waziri mkuu,  Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la mbunge wa Kwela aliyehoji Serikali ina mpango gani katika zao la mahindi katika kipindi ambacho wakulima wanaendelea kutafuta masoko.

Mbunge huyo amehoji namna Serikali ilivyojipanga ili kuziwezesha taasisi za Serikali kama NFRA  ziweze kununua mahindi ya wakulima.

Majaliwa amesema uzalishaji wa mahindi umekuwa mkubwa katika mikoa inayozalisha mahindi hivyo wameimarisha kitengo cha hifadhi ya chakula.

Amesema NFRA imepewa fedha za kwenda kununua mahindi  kumwezesha mkulima  ajikimu hadi msimu ujao ingawa uwezo si mkubwa.

"Nilibaini kuwa uwezo wao ni mdogo na nikapokea malalamiko ya wananchi kwamba kituo cha kupokea mahindi kiko mbali, kwa hiyo tumeamua kuanzia sasa kila halmashauri itapaswa iwe na kituo japo kimoja cha kupokea mahindi ili kuharakisha ununuzi wa zao hilo," amesema Majaliwa.

Amesema kwa sasa NFRA na bodi ya mazao mchanganyiko wamefungua milango kwa yeyote anayetaka kuuza mazao nje ikiwemo nchi za Zambia, Congo, Msumbiji au Malawi.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.