Serikali yajipanga kuilipa Indiana mabilioni ikishindwa kesi

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeridhia kwa maandishi katika Baraza la Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kulipa fidia ya Dola milioni 109 za Marekani (Sh260 bilioni) kwa kampuni ya Indiana Resources endapo itashindwa maombi ya kupinga malipo hayo.

Serikali inaomba kubatilishwa utekelezaji wa hukumu chini ya kifungu cha 50(2)(a) na (b) cha Mkataba wa ICSID ikiwasilisha hoja 15, ikipendekeza kufuta hukumu ya kulipa fidia ya kiasi hicho cha fedha.

Hukumu iliyotolewa na ICSID Julai 14, mwaka huu iliitaka Serikali ya Tanzania kulipa kiasi hicho cha fedha kwa kampuni ya madini ya Indiana Resources iliyokuwa ikimiliki leseni ya kuhodhi ardhi katika eneo la Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill, uliokuwa Wilaya ya Nachingwea.

Kwa mujibu wa taarifa ya jana Desemba 27, 2023 ya Mwenyekiti Mtendaji wa Indiana, Bronwyn Barnes, Tanzania kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imethibitisha kwa kampuni hiyo na baraza hilo kwamba itakuwa tayari kulipa kiasi hicho ndani ya siku 45 bila masharti baada ya uamuzi wa mwisho wa ICSID.

Hata hivyo, Barnes alisema kiasi kinachotakiwa kulipwa ni Dola milioni 118 (Sh300 bilioni).

“Haya ni matokeo mazuri kwa wadai ambayo yanatuletea hatua kubwa ya kurejesha deni kamili kama ilivyoainishwa katika tuzo ambayo sasa inafikia zaidi ya Dola milioni 118," amesema Barnes alipohojiwa na tovuti ya ukusanyaji wa habari za masoko ya hisa, The Market Bull.

Akizungumzia suala hilo, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniphace Luhende ameiambia Mwananchi Digital kuwa;

“Ukweli ni kwamba, Serikali imewasilisha maombi ya kupinga tuzo. Hii ni nafasi ya mwisho kwa Serikali kuipinga, endapo itashindwa itabidi kulipa kama ilivyoamriwa.”

“Hata hivyo, maombi bado hayajasikilizwa. Baraza la ICSID lilitaka Serikali kuweka ahadi kwamba itakuwa tayari kulipa endapo maombi ya kupinga tuzo hayatafanikiwa. Ndicho kilichofanyika,” amesema.

Luhende amesema, “Hakuna fedha yoyote iliyolipwa kwa sasa. Kila kitu kinasubiri uamuzi wa maombi. Tunatarajia yatasikilizwa kati ya Juni au Julai, 2024 na uamuzi kutolewa ndani ya miezi mitatu hadi minne baada ya kusikilizwa.”

Kuhusu ongezeko la deni, Luhende alisema kiasi halisi kitajulikana baada ya kuamuliwa maombi ya pingamizi.

Amesema Serikali inapinga kiasi hicho kilichotolewa na baraza na kwamba, "Kwa sasa wadai wanapiga hesabu za riba."


Kiini cha kesi

Msingi wa madai hayo unatokana na ukiukwaji wa Mkataba wa Uwekezaji (BIT) iliyosaini na Uingereza na Ireland ya Kaskazini mwaka 1994 ambao unahusisha wanahisa wenza wa Indiana Resources waliomiliki leseni hiyo.

Kwa mujibu wa Indiana inayomiliki asilimia 62.4 ya hisa za kampuni hizo mbili; Ntaka Nickel Holdings Ltd na Nachingwea UK Limited, walishawishi Serikali kurejesha leseni yao, lakini haikuwezekana kutokana na marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017 iliyozifuta.

Kwa mujibu wa mtandao wa asasi za kiraia zinazochambua Mikataba ya Kimataifa ya Biashara na Uwekezaji (Tatic), tangu mwaka 1965 hadi 2019, Serikali imeshasaini mikataba 20 ya BITs ikiwamo inayoendelea na utekelezaji wake hadi sasa, huku Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikishauri maboresho.

Serikali imeshakiri na kuanza kulipa fidia ya Dola milioni 165 (Sh380 bilioni) kwa Kampuni ya Eco Energy Group iliyoshinda kesi dhidi ya uamuzi wa kupokwa hatimiliki ya hekta 20,400 za mradi wa sukari Bagamoyo ikiwa ni ukiukwaji wa mkataba wa aina hiyo kati ya Tanzania na Sweden.