Serikali yakamilisha ujenzi shule Rombo
Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Shimbi Kwandere, wilayani humo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Shule mbili za kidato cha tano na sita za Mahida na Keni zilizoanzishwa kwa nguvu za wananchi na kushindwa kuendelea kwa zaidi ya miaka 10 wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro zimeanza kupokea wanafunzi wa kike wa kidato cha tano mwaka huu baada ya serikali kumalizia ujenzi wake.
Rombo. Shule mbili za kidato cha tano na sita za Mahida na Keni zilizoanzishwa kwa nguvu za wananchi na kushindwa kuendelea kwa zaidi ya miaka 10 wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro zimeanza kupokea wanafunzi wa kike wa kidato cha tano mwaka huu baada ya serikali kumalizia ujenzi wake.
Ujenzi wa shule hizo ulisimama kwa zaidi ya miaka 10 tangu kipindi cha aliyewahi kuwa mbunge wa Rombo, Basil Mramba, lakini Serikali ilipeleka fedha zikiwamo Sh300 milioni kwa shule yasekondari Keni ajili ya umaliziaji wa shule hizo na sasa zimeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.
Katika shule ya Sekondari Mahida, Serikali ilitoa zaidi ya Sh130 milioni kwa ajili ya umaliziaji wa jengo la bweni la wanafunzi wa kike ambalo litakuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 80 kwa wakati mmoja.
Akizungumza na wananchi jana Septemba 27 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Shimbi kwandere, wilayani humo, Mbunge wa Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema serikali ya awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi katika kuimarisha miundo mbinu ya elimu.
Profesa Mkenda, amesema wakati alipochaguliwa kuwa mbunge wa Rombo, wilaya hiyo ilikuwa na shule mbili pekee za kidato cha tano na sita ambazo ni Tarakea na Mkuu Day na kwa sasa Serikali imekamilisha shule mbili za Mahida na Keni.
"Kazi ya Serikali yetu ni kuimarisha miundo mbinu ya elimu, ufundishji madarasani na kutoa elimu iliyo bora kwa Watanzania wote na mnajua Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameweka vipaumbele vingi katika serikali yake lakini kikubwa zaidi ni kwenye elimu.
"Wakati nachukua ubunge shule ya sekondari Keni na Mahida kwa zaidi ya miaka 10 zilishindwa kumalizika na zilibaki pale pale alipoziacha Mramba, lakini leo tumemalizia alipoachia Mramba na wanafunzi wa kidato cha tano wameingia madarasani," amesema Profesa Mkenda
Amesema kwa muda mrefu zhule za Keni, Shimbi, Mahida zilikuwa hazijaendelezwa, lakini sasa zimekamilika.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wameishukuru Serikali pamoja na Profesa Mkenda kwa kuweka msukumo mkubwa katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa ipasavyo katika wilaya hiyo ikiwemo miradi ya elimu.
"Kwa hili la umaliziaji wa shule mbili za Mahida na Keni sekondari serikali imefanya jambo kubwa sana, tunaishukuru kwa umaliziaji wa majengo ya shule hizo mbili maana kwa zaidi ya miaka 10 tulikuwa hatujui mwafaka wa haya madarasa," amesema Amina Tesha, mkazi wa Shimbi.
Naye Gideon Athanas, mmoja wa wananchi wa Shimbi Kwandere amasema uwepo wa shule hizo utasaidia kuongeza ufanisi wa elimu katika wilaya hiyo.
"Shule hizi tuliwekeza kwa nguvu zetu wenyewe lakini ilifika mahali tukachoka kabisa na ujenzi ukawa umesimama kwa muda mrefu sana, lakini leo hii tunaishukuru serikali kwa uamuzi wa kufufua shule hizi kuwa na kidato cha tano," amesema.