Serikali yakataa ombi Mkwawa kuwa chuo kikuu

Naibu Waziri wa Elimu, Omar Kipanga.

Muktasari:

  • Naibu waziri amesema kwa sasa chuo hicho kitaendelea kuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Dodoma. Serikali haina mpango kukipandisha hadhi Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa kilichopo Iringa na kuwa chuo kikuu.

Hata hivyo, Serikali imeahidi kuendelea kukifanyia ukarabati ikiwemo majengo na miundombinu mingine kwa ajili ya kukifanya kiendelea kuwa bora zaidi.

Kauli hiyo, imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Omar Kipanga bungeni leo Jumatatu Novemba 5, 2023 wakati akijibu swali la msingi na nyongeza lililoulizwa na Mmbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rita Kabati.

“Ni kweli kama alivyosema mbunge huyo kile chuo kina watumishi 231 na karibu maprofesa 70 lakini kati ya hao hakuna profesa hata mmoja aliyeajiriwa na chuo hicho isipokuwa wote wanatoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” amesema Kipanga.

Awali, Kabati ameuliza Serikali inampango gani wa kupandisha Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa kuwa chuo kikuu kamili?

Mbunge huyo amesema kwa sasa Chuo cha Mkwawa kina miundombinu inayojitosheleza kwa ajili ya kupandishwa hadi na kuwa chuo kikuu ikiwemo idadi kubwa ya watumishi na maprofesa.

Naibu Waziri amesema Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu vya Tanzania na Mwongozo kuhusu Vyuo Vikuu Tanzania uliotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania mwaka 2019.

Amesema kwa sasa Serikali inaendelea kukiimarisha Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa kama Taasisi ya Elimu ya Juu chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kukifanya kuwa chuo kikuu kinachojitegemea.

Ameliambia bunge kuwa, Serikali itakipandisha hadhi kitakapokidhi taratibu zilizowekwa na nchi na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.