Serikali yakuna kichwa vyanzo vipya vya mapato

Serikali yakuna kichwa vyanzo vipya vya mapato

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imesema ipo haja ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato kuongezea katika mgawo wa sasa kupitia mfuko wa barabara ili kufanikisha ugharamiaji wa mtandao wa barabara hizo.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema ipo haja ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato kuongezea katika mgawo wa sasa kupitia mfuko wa barabara ili kufanikisha ugharamiaji wa mtandao wa barabara hizo.

Hatua hiyo inatokana na hali ya barabara vijijini hairidhishi ambapo bado vipo vijiji ambavyo havina barabara kabisa.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 10, 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema barabara nyingi zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) zina hali mbaya ambapo kwa sasa mtandao wa barabara zilizo chini ya Tarura una urefu usiopungua kilomita 108,946.2 ambazo zinaunganisha maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini.

“Hadi Desemba 2020, mtandao wa barabara zilizo chini ya Tarura wenye kiwango cha lami ulifikia kilometa 2,250.69  sawa na asilimia 2.1 tu, changarawe kilometa 27,809.26 (asilimia 25.6) na udongo kilometa 78,886.25 (asilimia 72.4).”

“Hali hii ya barabara ina madhara makubwa sana kwa jamii yetu kwani baadhi ya akina mama wajawazito wanapoteza maisha kwa kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya,” amesema Mwigulu.

Amesema wapo wengine ambao wanajifungulia njiani kutokana na kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya na kwamba wapo baadhi ya wanafunzi wanaosombwa na maji na kufariki kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara, hususan katika maeneo ya vijijini.