Serikali yakunjua makucha mgomo wa hospitali binafsi

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma za afya na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) leo Ijumaa  Machi mosi 2024 mkoani Lindi. Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

 Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amewataka Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya Tanzanja (Aphfta) kuhakikisha wanaheshimu leseni zao kwa kutoa huduma wakati majadiliano yakiendelea

Dar/Lindi. Wakati Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya Tanzanja (Aphfta) wakisitisha kutoa huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Serikali imewaagiza watoa huduma hao kurudi mezani kufanya mazungumzo na kamati iliyoundwa huku wakiendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Serikali imezitaka hospitali binafsi kupokea wagonjwa kulingana na masharti ya leseni na usajili wa hospitali hizo.

Kauli ya Serikali inakuja wakati ambapo leo Machi mosi, 2024 baadhi ya hospitali ikiwamo ya Kairuki, Regency, TMJ, Hospitali ya Ekenywa za jijini Dar es Salaam zikisitisha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF.

Mgomo huo ni kufuatia tangazo la saa 48 la Aphfta ikiitaka Serikali warudi meza moja ndani ya muda huo kufikia mwafaka kabla ya kuwasitishia huduma wagonjwa wenye kadi za NHIF na kwa wale wanaoendeela kupata huduma wakiwemo wagonjwa wa kulazwa watapelekwa hospitali za umma kuendelea na matibabu.

Kiini cha mgororo mgomo huo ni watoa huduma hao kugomea maboresho ya kitita kipya cha NHIF kwa madai gharama za huduma zilizopangwa na NHIF zitawafanya kushindwa kujiendesha.

Kauli ya Serikali

Leo Ijumaa, akizungumza na waandishi wa habari mkoani Lindi, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka watoa huduma binafsi kuendelea kufanya majadiliano na kamati aliyoiunda wakati wakiendelea kuwahudumia wananchi.

“Nisisitize majadiliano yatafanyika wakati huduma zinaendelea kutolewa, tuongee wakati huduma zikiendelea kutolewa. Natoa rai kwa hospitali zote zilizositisha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF ziendelee kuwahudumia wanachama hao.

“Toeni huduma, ni wiki moja mbili tatu njooni tukae Serikali tumeweza kutoa huduma kwa kitita kipya changamoto ni moja mbili tatu, uzuri tunakwenda  mwaka mpya wa bajeti 2025,2026  bado fursa ipo kwahiyo majadiliano yatafanyika wakati huduma zinaendelea,” amesema.

“Namwelekeza Msajili wa Hospitali Binafsi kutoa notice na kuchukua hatua mara moja kwa watoa huduma wote ambao kwa namna moja watakiuka sheria anazozisimamia,” amesema Ummy.

 “Ninavielekeza vituo/hospitali zote binafsi na za umma nchini kuendelea kuwapokea wagonjwa wa dharura pindi wanapofika katika vituo vyao kwa kuwa hili ni takwa la Sheria namba 151 ya Usajili wa Vituo Binafsi vya kutolea huduma na kanuni yake namba 32. Kutowapokea wagonjwa hao ni kuvunja Sheria husika.”

Pia, ametoa maagizo kwa wakuu wa mikoa wahakikishe wanaendelea kusimamia kwa karibu utoaji wa huduma za afya katika maeneo yao ikiwemo kusimamia maelekezo haya kupitia wataalam wa afya katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri kuchukua hatua stahiki kulingana na kanuni na Sheria zilizopo kwa kushauriana na Wizara ya Afya.

Waziri Ummy amesema bado milango ya wizara ipo wazi na wanawakaribisha watoa huduma binafsi kuendelea kujadiiliana maeneo ambayo hawajaridhika kwa hoja na si kupinga kwa maneno.

Hoja alizohitaji Ummy zipingwe kwa hoja na Aphfta ni gharama za dawa, uendeshaji pamoja na faida ambayo kamati iliridhishwa nayo akiwataka watoa huduma hao wasikatae vitu kwa ujumla.

“Aphfta watuambie kama vigezo vilivyowekwa na kamati hawakubaliani nazo, hakuna vigezo vingine dawa umenunua kiasi gani, gharama za uendeshaji na faida waje mezani waseme mmetuwekea faida ndogo, waje mezani watuambie dawa haiuzwi bei hii ushahidi tunao sio waseme hatutaki kitita leteni hoja zenu mezani,”amesema.

Kiongozi huyo wa sekta ya afya amesema Serikali imeielekeza NHIF kuendelea na kitita chao lakini wazingatie maoni na mapendekezo ya kamati.

Amesema gharama ya kumuona daktari NHIF wamebadilisha na kurudi kwenye mapendekezo ya kamati, hivyo maboresho yaliyofanyika ni kupata na kukosa huku akisisitiza vipo vitu NHIF imepoteza na Aphfta wakubali kupoteza baadhi ya vitu.

“Tumewaelekeza NHIF kuendelea kupokea maoni ya wadau  kuhusu kitita wakati wa utekelezaji,tumewasiliza sana Aphfta mimi na jopo langu tumewa ‘accommodate’ sana tangu mwaka 2022 Agosti ni kuchelewa tu na tumekuwa wavumilivu, wizara inaendelea kusisitiza umuhimu wa majailiano katika suala hili ili kupata suluhu ya jambo hili,” amesema Ummy.

Waziri Ummy amesema baada ya kupata taarifa ya kamati, aliitisha kikao akiwa na timu ya watalamu wa wizara ya afya, wataalamu wa NHIF, wamiliki wa vituo binafsi, kamati ya afya chini ya Bakwata, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanznaia (Tira), Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na Tume ya Kikirsto ya Huduma za Kijamii na taarifa ya kamati hiyo ikawasilishwa.

Ummy amekiri baada ya kuwasilishwa taarifa hiyo hakuna mdau yeyote aliyepinga badala yake wadau hao walimuomba wao wakafanye hesabu zao kwanza.

“Pia, suala hili tuliwasilisha bungeni kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi kupata maoni na ushauri wao jambo jema hakuna aliyeweza kujenga hoja,” amesema Ummy.