Serikali yalifungia gazeti la Uhuru kwa siku 14

Muktasari:
- Serikali imesitisha kwa muda wa siku 14 leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la UHURU kuanzia kesho Alhamisi Agosti 12, 2021
Kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 9(b) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016 nimeamua kusitisha kwa muda wa siku kumi na nne (14) leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la UHURU kuanzia tarehe 12 Agosti, 2021.
Uamuzi wa kusitisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la UHURU unatokana na gazeti hilo toleo Na. 24084 katika ukurasa wa mbele kuchapisha habari inayosomeka ‘Sina wazo kuwania urais 2025 – Samia’, habari ambayo imeendelea ukurasa wa pili.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, imebaini kuwa habari hiyo ina upungufu wa kisheria na weledi wa taaluma ya Uandishi wa Habari kwa kutoa taarifa za uongo dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kinyume na kifungu cha 50(1)(a),(b), na (d) na kifungu cha 52(d) na (e) vya Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016. Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hajatoa matamshi yoyote ambayo yanaeleza kutokuwa na wazo la kuwania urais mwaka 2025.
Pia, kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016, ikiwa gazeti la UHURU halitaridhika na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari linayo haki ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya Habari.
Ofisi ya Idara ya Huduma za Habari inaamini kuwa adhabu hii itatoa nafasi ya kuboresha masuala yanayohusu weledi wa Uandishi wa Habari na utekelezaji wa masuala yote yanayohusu uzingatiaji wa Sheria, maadili na kanuni kwa gazeti hilo.
Aidha, Vyombo vya Habari vyote mnakumbushwa kuzingatia Sheria, maadili, kanuni na miongozo mbalimbali inayohusu tasnia ya habari, ili kulinda taaluma na kuleta ustawi wa jamii.
Imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Gerson Msigwa