Serikali yashtukia uingizaji vitabu visivyo na maadili shuleni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Francis Michael
Dodoma. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imebaini uwepo wa shule zinazoingiza na kutumia vitabu ambavyo maudhui yake yanakinzana na mila, desturi, miongozo na tamaduni za Mtanzania.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya baadhi ya mitandao ya jamii kusambaza vitabu vinavyokinzana na mila na tamaduni za Tanzania, ikiwemo kuhamasisha mahusiano ya jinsia moja.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Francis Michael alisema katika kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu nchini unazingatia ubora, masilahi ya Taifa, mila, desturi na tamaduni za Mtanzania, ilitoa waraka namba nne wa mwaka 2014, sheria na miongozo inayohusu elimu.
Alisema vyote vililenga kuhakikisha kuwa vitabu vya ziada na kiada vinavyotumika katika shule zilizosajiliwa nchini, vinaendana na mila, destruri na utamaduni wa nchi.
“Katika kusimamia utekelezaji wa waraka huo, wizara imebaini kuwa kuna shule zinazoingiza na kutumia vitabu ambavyo maudhui yake yanakinzana na mila na desturi, miongozo pamoja na tamaduni za Mtanzania.
“Vitabu hivyo visivyoruhusiwa kutumika orodha yake itatangazwa au kutolewa baada ya waziri mwenye dhamana kupitia ripoti na kuvipiga marufuku,” alisema Dk Francis.
Aliwataka wamiliki na waendeshaji wa shule zote za umma, binafsi zilizosajiliwa nchini kufuata na kuzingatia waraka namba 4 wa mwaka 2014, sheria na miongozo inayosimamia elimu, vinginevyo hatua kali, ikiwamo kufuta usajili wa shule zinaweza kuchukuliwa.
Aidha, Dk Michael alisema ripoti ya timu ya uchunguzi ya wizara hiyo kuhusu tabia chafu na upotoshaji wa maadili itatolewa hivi karibuni.
Wadau wanena
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Nchini (TEN/MENT), Ochola Wayoga alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo ni vyema vitabu vyote kabla ya kuingia shuleni, vihakikiwe na maofisa elimu nchini na kisha waweke sahihi.
“Vitabu hivi vingi vinaingia kwa msaada, sijui shirika hili limeleta msaada, mengine ni kama haya ya kwetu, lakini wanakuwa hawajapitia vitabu vya kupelekwa shuleni. Vinakuja kwa mtindo wa kuongeza uelewa wa Kiingereza,” alisema.
Mdau wa elimu na mbunge wa viti maalumu (CCM), Dk Thea Ntara alipongeza hatua ya wizara, lakini akataka Serikali kufanya uchambuzi wa kina wa vitabu vinavyouzwa na watu binafsi kwa ajili ya matumizi mashuleni. “Sisi wadau wa elimu tunangoja tupate orodha ya vitabu, lakini na waandishi wa hivyo vitabu ikibidi wasiwaache hivi hivi…Sheria iwe kali kwa kuandika kitabu cha kubadilisha kabisa mtoto kichwa chake.
“Hawa watu wapate adhabu kubwa, wafungiwe kampuni zao na wapelekwe mahakamani,” alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema kabla ya kusambaza vitabu, vikiwemo vile vinavyoandikwa nje ya nchi, ni lazima Serikali ijiridhishe maudhui yaliyomo.
“Sisi wenyewe Watanzania tunatakiwa tujilaumu kwa kutochuja vitabu vinavyotakiwa kuingia katika soko.
Ifanyike kama ambavyo tunafanya kwenye muziki na dawa ambapo wamekuwa wakizuia na wahusika kufungiwa,” alisema.