Serikali yataja mikakati kudhibiti simu kwa watoto
Muktasari:
Kutokana na kuongezeka kwa watoto wanaotumia simu za watu wazima, Serikali imesema inatarajia kuja na programu ya ‘TotoSimu’ itakayokuwa na video mbalimbali zikiwemo za michoro ‘animation’ zenye kutoa elimu kwa kundi hilo.
Dar es Salaam. Kutokana na kuongezeka kwa watoto wanaotumia simu za watu wazima, Serikali imesema inatarajia kuja na programu ya ‘TotoSimu’ itakayokuwa na video mbalimbali zikiwemo za michoro ‘animation’ zenye kutoa elimu kwa kundi hilo.
Michoro hiyo imetajwa kuwa itasaidia kuwapa watoto elimu sahihi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia, mafundisho ya kimasomo, malezi bora ikiwa ni sehemu ya programu ya malezi na makuzi jumuishi ya watoto.
Pamoja na hayo Serikali inaandaa wiki ya wabunifu na waleta ufumbuzi ili wataalamu wa Serikali wasikie na kuona ni mbinu zipi za kibunifu zinafaa kutumika kwa jamii ili ielewe na kuweza kuchukua hatua kupitia bunifu hizo.
Hayo yamesemwa leo Machi 9, 2022 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalu, Dk Doroth Gwajima wakati alipotembelea maonyesho yaliyoandaliwa na muungano wa asasi za kiraia (Mkuki Coalition) katika muendelezo wa siku ya wanawake duniani ambapo ameshuhudia bunifu mbalimbali za teknolojia ya mawasiliano zinavyofanya kazi kumsaidia mwanamke katika maeneo mbalimbali.
Alisema watoto wengi wamekuwa wakitumia simu za wazazi wao kuangalia mambo ya watoto ikiwemo katuni au kufanya mazoezi ya shule, hivyo uwepo wa simu hizo itamwezesha mtoto kutumia program zinazomhusu pasipo kuona vitu visivyomfaa pamoja na kupiga namba za dharura 116 kuripoti vitendo vya ukatili iwapo atafanyiwa.
“Tutengeneze program za watoto kwenye simu hususani zile zinazotumiwa na watoto mfano tunaziita ‘TotoSimu’ hizi ni simu za watoto pekee zenye kule anapata meseji inayomwelekeza kununua program mpya na mzazi unanunua pile unayoona itamfaa inakaa kwenye simu yake.
“Haya hayakwepeki lazima twende huko ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan mwaka jana alizindua program ya malezi na makuzi jumuishi ya watoto anataka kusuka taifa, hawa wanaochipuka huku tuweke nguvu kubwa zaidi ili tuwe na Watanzania wa kesho ambao tokea mwanzo wana misingi ya kulelewa kwa kuwa hawakujifunza mambo mabaya,
“Unajua mtoto ukishajifunza mambo mabaya kwenye mafaili kichwani mwake yanadumu na ni ngumu kuja kufuta,” amesema Waziri Gwajima.
Amesema Serikali inafikiria kupata wafadhili, wadau ili kushirikiana katika hilo, “Tuwe na ‘TotoSimu’ isiwe tena hofu umelala mwanao kachukua simu yako unaanza kukosa usingizi, akiwa na simu yake analimit ya kuona mambo hasa utakayochagua wewe mzazi yanayomjenga ajue njia ipi nzuri ya kupita na ipi mbaya itampa matokeo mabaya.”
Waziri Gwajima amesema wadau hao wana bunifu nyingi zinazojibu kiu ya Serikali hivyo ni wajibu wa Serikali kushirikiana na wadau ili kupata suluhu kwa muda mfupi, “Sauti kama hizi kuna local redio kwenye halmashauri zikipewa Tanzania nzima elimu itafika kwa muda mfupi kuliko kutumia fedha nyingi kwenye semina ambazo matokeo yake hayaji kwa muda mfupi.
“Tuache mchezo, tuna wadau wengi wapo wanafanya hizi kazi na sisi Serikali tupo bize tunafanya kitu kilekile tujipime tuone hawa watengeneza bunifu wapo wangapi wanaunganaje kuwa chombo kikubwa ili kuleta suluhisho kwenye jamii.”
Ofisa Mawasiliano wa Tai Tanzania, Mariam Mhina amesema wamefanikiwa kutengeneza picha jongefu ‘animation’ 12 zenye mafundisho mbalimbali na wamewafikia wanafunzi 8000 na kwenye jamii zaidi ya watu 2,000,000 na mikoa saba kwa mwaka jana.
Amesema picha hizo zenye mafunzo mbalimbali wamekuwa wakiziweka kwenye mtandao ya youtube ‘Tai Tanzania’ na program zinazomwezesha mtoto kuangalia hata kama hana mtandao.
“Sisi Tai tunatengeneza animation zenye mambo tofauti, ipo ya Shujaa inayoonyesha jinsi gani ukatili wa kijinsia ulivyokuwa na matokeo mabaya kwenye jamii na kama wazazi tunaweza kufanya nini ili kuwasiaida watu wanaokumbana na ukatili wa kijinsia,” alisema Mariam.
Mkurugenzi wa Shirika la Tangible Initiative for Local Development Tanzania, Wakili Geline Fuko ameipongeza Serikali kupitia wizara hiyo kuweza kuzifikia taasisi hizo na kuanza mchakato wa kuwaratibu ili kufanya kazi kwa pamoja.