Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yataja mikakati kukabili sikoseli

Mratibu wa Ugonjwa wa Sikoseli Taifa, Dk Asteria Mpoto, akieleza namna jamii inavyoweza kukabiliana na ugonjwa wa sikoseli nchini Tanzania. Picha na Mbonea Herman

Muktasari:

  • Ugonjwa huo unadhibitiwa ukigundulika mapema na mgonjwa kufuatilia kliniki kila mwezi.

Tanga. Takribani watoto 14,000 huzaliwa na ugonjwa wa sikoseli kila mwaka nchini, huku maelfu ya wengine wakiendelea kuishi na changamoto za maumivu ya mara kwa mara, kulazwa hospitalini na kukosa masomo kwa wanafunzi.

Licha ya hali hiyo, wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo unaweza kudhibitiwa, iwapo utagundulika mapema na wagonjwa wakapatiwa huduma stahiki, kama inavyosimuliwa na Stella Nyakanga, mzazi wa mtoto mwenye ugonjwa huo.

Katika simulizi yake leo, Ijumaa Juni 19, 2026, Stella anayeishi Tanga, amesema awali hakujua kama mwanawe anaumwa ugonjwa huo, lakini mara kwa mara aliugua bila kujulikana ugonjwa unaomsumbua.

“Mara kwa mara alikuwa anaumwa bila sababu kufahamika. Nilistuka sana nilipoambiwa ana sikoseli kwa sababu watoto wangu wengine hawakuwa na tatizo hilo,” amesema.

Hali ya kuugua mara kwa mara, amesema ikamletea tatizo hata wakati wa masomo yake pale alipoanza shule. Kuna wakati alilazimika kuacha kuhudhuria masomo.

Mazingira hayo, amesema ndiyo yaliyomfanya kwenda kupimwa magonjwa mbalimbali na baadaye akabainika kuwa na ugonjwa huo.

Amesema walianza kuhudhuria kliniki maalumu ya sikoseli katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, hali yake ilianza kuimarika.

“Kwa sasa anaweza kucheza na kusoma vizuri zaidi. Tunatumia bima ya afya na tunafuatilia kliniki kila mwezi,” amesema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya damu katika hospitali hiyo, Eveline Banda, amesema dalili za sikoseli huanza kuonekana mtoto akiwa na umri wa miezi mitatu hadi sita.

Dalili hizo, amesema ni pamoja na maumivu ya mara kwa mara, kuvimba vidole, maambukizi ya mara kwa mara na upungufu wa damu.

“Uchunguzi wa mapema ni muhimu ili mtoto aanze matibabu kwa wakati na kupunguza madhara ya ugonjwa,” amesema.

Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza Mkoa wa Tanga, Dk Elisey Magiri, amesema hadi Aprili 2026 wagonjwa 413 walikuwa wakifuatiliwa katika vituo vya afya mkoani humo.

Ameeleza changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa jamii, unyanyapaa na kuchelewa kufika hospitalini.

Hata hivyo, amesema Serikali imeanzisha kliniki maalumu za sikoseli na kuboresha upatikanaji wa dawa muhimu.

Kwa upande wake, Mratibu wa Taifa wa Ugonjwa wa Sikoseli, Dk Asteria Mpoto, amesema takribani watoto 14,000 huzaliwa na ugonjwa huo kila mwaka nchini, huku asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania wakiwa na vinasaba vya sikoseli.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa kuwa na ugonjwa huu, lakini huduma za uchunguzi na matibabu zimeendelea kuboreshwa,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa upimaji wa vinasaba kabla ya ndoa, ufuatiliaji wa kliniki, lishe bora na kuwahi hospitalini mara dalili zinapoonekana.

Dk Asteria, amesema sikoseli inaweza kudhibitiwa ikiwa itagundulika mapema na wagonjwa wakafuata ushauri wa wataalamu wa afya.