Prime
Janga la sikoseli, utafiti wafichua siri
Muktasari:
- Licha ya maendeleo yaliyofikiwa katika tiba na utambuzi wa ugonjwa wa selimundu maarufu (sikoseli) wataalamu wa afya wanaonya kuwa idadi kubwa ya watoto bado wanachelewa kugundulika kuwa na ugonjwa huo
Dar es Salaam. Kwa miaka mingi, kijiji kimoja kilichopo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, karibu na mpaka wa wilaya za Mpwapwa na Kilosa mkoani Morogoro, kiligubukwa na simanzi, hofu na maswali yaliyokosa majibu.
Katika familia moja maskini, mama alikuwa amejifungua watoto 10, lakini sita kati yao walifariki dunia wakiwa wadogo.
Kila mtoto alionekana mwenye afya njema alipozaliwa, lakini baada ya muda alianza kuugua mara kwa mara, kupata homa za vipindi, maumivu makali mwilini, upungufu wa damu na hatimaye kupoteza maisha.
Kadiri vifo hivyo vilivyoendelea kujirudia, familia hiyo ilianza kutengwa na baadhi ya watu walioamini kuwa huenda ilikuwa imekumbwa na laana au nguvu za ushirikina.
Waganga wa jadi waliitwa, dua na maombi mbalimbali yakafanyika, lakini hakuna aliyefanikiwa kubaini chanzo cha tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wadau Wanaoshughulika na Ugonjwa wa Sikoseli Tanzania (TSDA), Dk Elisha Osati (kulia) akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na mwandi wa Mwananchi Herieth Makwetta.
Mwaka 2023, wakati akiendelea na tafiti zake kuhusu ugonjwa wa selimundu, maarufu kama sikoseli, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji na magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Elisha Osati alipata taarifa kuhusu familia hiyo na kuamua kuifuatilia.
Baada ya kufika kijijini hapo, alianza kuchunguza historia ya ugonjwa huo katika familia, kusikiliza simulizi za mama huyo na kuwafanyia tathmini watoto waliokuwa bado hai.
Matokeo ya uchunguzi wake yalibadili mtazamo wa familia na jamii iliyokuwa imeizunguka.
“Watoto hawa hawakuwa wamelogwa wala familia haikuwa na laana kama ambavyo wanakijiji waliamini. Walikuwa wanaishi na ugonjwa wa sikoseli,” anasema Dk Osati.
Ugunduzi huo uliwaondolea mzigo mkubwa wa kisaikolojia wazazi hao na kutoa majibu ya kisayansi kuhusu vifo vya watoto wao.
Hata hivyo, simuliz hiyo ya Dk Osati si ya kipekee, kwa kuwa maelfu ya familia nchini zinakabiliwa na changamoto kama hizo kutokana na ugonjwa huo wa kurithi.
Tanzania miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika hivi karibuni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Sikoseli Duniani yanayoadhimishwa kila ifikapo Juni 19, Dk Osati ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wadau Wanaoshughulika na Ugonjwa wa Sikoseli Tanzania (TSDA), anasema ugonjwa huo bado ni tishio kubwa kwa afya ya watoto nchini.
Anasema sikoseli ni ugonjwa wa kurithi unaoathiri chembe nyekundu za damu.
Anasema kwa mtu mwenye afya ya kawaida, chembe hizo huwa na umbo la duara linalowezesha kusafiri kwa urahisi katika mishipa ya damu na kusambaza oksijeni mwilini.
Kwa wagonjwa wa sikoseli, anasema chembe hizo hubadilika na kuwa na umbo la mundu, hali inayozifanya kushindwa kusafirisha oksijeni kwa ufanisi na wakati mwingine kuziba mishipa midogo ya damu.
“Matokeo yake ni maumivu makali, upungufu wa damu, maambukizi ya mara kwa mara na matatizo mengine makubwa ya kiafya,” anasema.
Anafafanua kuwa mtoto hupata ugonjwa huo pale anaporithi chembe yenye kasoro kutoka kwa baba na mama wote wawili.
Changamoto kubwa ni kwamba watu wengi wenye chembe moja ya sikoseli hawaoneshi dalili zozote, hivyo huendelea kuishi bila kujua hali zao za vinasaba.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wadau Wanaoshughulika na Ugonjwa wa Sikoseli Tanzania (TSDA), Dk Elisha Osati akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na mwandi wa Mwananchi.
Tafiti zinaonyha Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo.
Inaelezwa takribani watoto 14,000 huzaliwa na sikoseli kila mwaka. Aidha, kati ya asilimia 15 hadi 23 ya Watanzania wana chembe moja ya ugonjwa huo bila kufahamu.
Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Kigoma, inatajwa kuongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha watu wenye vinasaba hivyo.
Dk Osati anasema hali hiyo inahusishwa kwa kiasi kikubwa na historia ya maambukizi ya malaria katika maeneo hayo.
Watu wenye chembe moja ya sikoseli huwa na kinga fulani dhidi ya malaria kali, jambo lililochangia kuendelea kuwepo kwa vinasaba hivyo katika jamii kwa vizazi vingi.
Maumivu makali na gharama kubwa
Dk Osati anasema mojawapo ya changamoto kubwa kwa wagonjwa wa sikoseli ni maumivu ya mara kwa mara yanayosababishwa na kuziba kwa mishipa ya damu. Baadhi ya wagonjwa hufananisha maumivu hayo na uchungu wa kujifungua.
Mbali na maumivu, Dk Osati anasema wagonjwa wanaweza kupata kiharusi, matatizo ya figo, macho, maambukizi ya mara kwa mara na hata kupoteza maisha mapema.
Kwa watoto wa kiume, anasema ugonjwa huo unaweza pia kusababisha kusimama kwa uume kwa muda mrefu bila sababu ya kawaida, hali inayohitaji matibabu ya haraka.
Anasema athari zake hazimkabili mgonjwa pekee bali familia nyingi hutumia sehemu kubwa ya kipato chao kugharamia matibabu, huku wazazi wakilazimika kukosa kazi mara kwa mara ili kuwahudumia watoto wao hospitalini.
“Unakuta mama hawezi kufanya kazi kwa uhuru kwa sababu mtoto anaumwa mara kwa mara. Hii inaathiri maisha na uchumi wa familia nzima,” anasema.
Matibabu na njia ya kujikinga
Ingawa bado hakuna tiba rahisi inayopatikana kwa wagonjwa wote, Dk Osati anasema ugonjwa huo unaweza kudhibitiwa kwa matibabu sahihi.
Huduma za matibabu hayo ni pamoja na kuongeza damu, kutibu maambukizi, kudhibiti maumivu na matumizi ya dawa maalumu kama Hydroxyurea, ambayo imeonyesha mafanikio katika kupunguza madhara ya ugonjwa huo.
Kwa wagonjwa wachache, anasema upandikizaji wa uloto wa mfupa unaweza kutoa tiba ya kudumu, lakini gharama zake ni kubwa na huhitaji mtoaji anayelingana kinasaba.
Anasema suluhisho la muda mrefu ni kuhakikisha wananchi wanapima hali zao za vinasaba mapema kabla ya kuingia kwenye mahusiano ya kudumu.
Kupitia kampeni ya “Vunja Mduara”, wataalamu wanahamasisha vijana kupima ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu uzazi na kupunguza uwezekano wa kuzaliwa kwa watoto wenye sikoseli.
“Hatulazimishi watu waachane. Tunataka wafanye maamuzi wakiwa na taarifa sahihi,” anasema.
Kadiri Tanzania inavyojiandaa kuadhimisha Siku ya Sikoseli Duniani Juni 19 mkoani Kigoma, wataalamu wanaendelea kusisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii, upimaji wa mapema na upatikanaji wa huduma bora za matibabu.
Ujumbe wao ni mmoja: wananchi wafahamu hali zao za sikoseli mapema ili kusaidia kuvunja mduara wa ugonjwa huo na kuokoa maisha ya vizazi vijavyo.