Wataalamu washauri wenza kupima sikoseli kabla ya ndoa

Muktasari:
Mkoa wa Tabora ni wa nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa sikoseli ukitanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kigoma.
Tabora. Wagonjwa 386 wa ugonjwa wa Sikoseli walilazwa wodi ya watoto mwaka 2022 kwa sababu ya changamoto za kiafya za ugonjwa huo na wengine 291 kuhudhuria Kliniki.
Akizungumzia ugonjwa huo Septemba 10, 2023 Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete, Dk Renatus Burashahu amesema kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu, wagonjwa 188 walilazwa wodi ya watoto na 133 walihudhuria Kliniki ya Sikoseli.
Ameeleza kuwa kutokana na idadi hiyo ya wagonjwa Mkoa wa Tabora unakuwa wa nne nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa hao ukitanguliwa na Dar es Salaam, Mwanza na Kigoma.
“Nchi yetu ni miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa wa Sikoseli ikiwa ni ya nne Barani Afrika na ya tano ulimwenguni ambapo inakadiliwa kuwa ni asilimia 20 ya Watanzania wanabeba vinasaba vya ugonjwa wa Sikoseli ambao unaongezeka mwaka hadi mwaka. Tatizo hilo linaonekana katika Hospitali ya rufaa Kitete kutokana na idadi kuongezeka kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma,”amesema
Dk Burashahu amesema kwa kuzingatia ongezeko la kupanda kwa takwimu za wagonjwa wa Sikoseli kidunia na Kitaifa, Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameungana kwa pamoja kuadhimisha mwezi wa kuijengea uelewa jamii ili ifahamu zaidi ugonjwa huo huku, kupima ugonjwa huo ili kuondokana na dhana potovu iliyozagaa miongoni mwao kuwa ugonjwa huo ni wa kurithi.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya Watoto Mkoa wa Tabora, Dk Amon Ryakitimbo ameishauri jamii hasa wanaotarajia kufunga ndoa waende hospitalini kupima ugonjwa wa Sikoseli ili wafahamu afya zao kabla ya kufunga ndoa .
“Ukichagua mwenza ambaye hana changamoto ya ugonjwa wa sikoseli, unakuwa umejiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata mtoto asiyekuwa na changamoto ya ugonjwa huo,” amesema
Amefafanua kuwa nia kubwa ya kupima ni kujua changamoto ya Sikoseli kama ni mbebaji wa kinasaba kuna njia ya kujikinga na madhara yanayotokana na ugonjwa huo.