Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yataja ukomo wa michango kidato cha tano

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba akizungumza wakati akijibu maswali kwenye kikao cha 43 cha mkutano wa 15 wa Bunge la bajeti unaoenndelea jijini Dodoma leo Juni 7,2024. Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • Serikali imeweka ukomo wa michango kwa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha tano nchini ili kuleta unafuu kwa wazazi.

Dodoma. Serikali imetoa ukomo wa michango kwa wanafunzi wanaojiunga na masomo ya kidato cha tano kuwa ni Sh80,000 kwa shule za bweni na Sh50,000 kwa shule za kutwa.

 Ukomo huo umetajwa leo Juni 7, 2024 na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde Mohamed Said Issa.

Mbunge huyo amehoji Serikali ina mpango gani wa kuleta unafuu wa gharama za michango ya kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza na cha tano.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema Serikali inatekeleza sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, ambalo pamoja na mambo megine inatamka kuwa Serikali itahakikisha kuwa elimu ya awali, msingi na sekondari inatolewa bila ada katika mfumo wa umma.

Aidha, amesema waraka wa elimu namba tatu wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa elimumsingi bila malipo, unabainisha majukumu ya wadau wote ikiwa ni pamoja  na utaratibu wa kuzingatia ili kupata kibali cha kukusanya mchango wa aina yoyote.

“Ili kuleta unafuu wa gharama za michango, Serikali imetoa maelekezo ya kujiunga na kidato cha tano katika shule zote za sekondari za Serikali Tanzania, ambapo ukomo wa michango hiyo ni Sh80,000 kwa shule za bweni na Sh50,000 kwa shule za kutwa,” amesema.

Aidha, wanafunzi wa kidato cha kwanza wanapokelewa kwa kuzingatia Waraka wa Elimu namba tatu wa mwaka 2016 wa elimumsingi bila ada, ambapo wanafunzi hawatikiwi kutoa mchango wowote bila kibali cha wakuu wa wilaya.

Katika maswali ya nyongeza Issa, alitaka kufahamu kama Serikali iko tayari kuainisha aina ya michango ambayo imeruhusiwa kuombewa kibali.

Amehoji iwapo Serikali iko tayari kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule kuwaruhusu wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuchangia michango hiyo kwa wakati, waendelee na masomo.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema waraka namba tatu umeeleza juu ya utaratibu wa kuomba michango na ni lazima kupata kibali cha mkuu wa wilaya.

Amesema michango hiyo inawezekana ikawa ni ile ya wazazi wenyewe au kupitia kamati za shule, hivyo wazazi wanakubaliana.

“Kwa mfano wanaweza wakataka kuwe na masomo ya ziada, michango ya uendeshaji wa shule ambapo ukomo umewekwa kwa shule za bweni,” amesema.

Aidha, Katimba amesisitiza maagizo kwa maofisa elimu na wakuu wa shule, kuwa hawaruhusiwi kuwakataa wanafunzi kwa sababu tu ya kukosa pesa za michango.

Amewataka wazazi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano kuwapeleka shule watoto wao hata kama hawajakamilisha michango.