Serikali yatakiwa kushirikisha wananchi ulinzi rasilimali
Muktasari:
- Utafiti wasisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kwenye mipango ya uendelezaji wa maliasili katika maeneo husika. Waziri Mchengerwa kuzindua kitabu cha utafiti huo.
Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa akitarajiwa kuzindua kitabu cha utafiti wa maliasili Aprili 4 mwaka huu, Serikali imetakiwa kushirikisha wananchi ulinzi wa maliasili.
Utafiti huo uliofanywa na watafiti kutoka vyuo vikuu vinne duniani ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika idara Jiografia, Sayansi ya Siasa na Kilimo na Uvuvi.
Utafiti huo uliofanyika katika wilaya tatu za mikoa ya Kusini ambazo ni Rufiji, Kilwa na Mtwara vijijini ulilenga kuangalia ongezeko la ushirikiano wa wadau katika uhifadhi wa maliasili na tija yake.
Akizungumza leo Aprili 2 jijini Dar es Salaam, Rasi wa ndaki ya sayansi za jamii, Profesa Christine Noe amesema utafiti huo ulioangalia maliasili za mazao ya bahari, wanyamapori na misitu, imebainika kuwa licha ya hamasa ya utunzaji wa mazingira, bado hakujawa na uwazi kati ya mifumo na jamii zilizo karibu na maliasili husika.
Profesa Chistine amebainisha kuwa utafiti huo umekuja na mapendekezo kadhaa ikiwemo Serikali kuhakikisha juhudi za kushirikisha jamii zinakwenda sambamba na kuwajengea imani kwamba ni wamiliki wa rasilimali hizo.
“Lazima Serikali iwafanye wanajamii wajione sehemu ya umiliki wa malisili husika, kinyume na hivyo mambo yanaweza kuwa tofauti wasiishie kutoshiriki bali hata kuhujumu.
“Pia Serikali ihakikishe kwamba faida zinazotokana na ushirikiano katika kuhifadhi zinagawanywa kwa usawa kwa wanajamii na kuepuka kufaidisha watu wachache,” amesema Profesa Christine.