Serikali yatanga operesheni tokomeza mifuko ya plastiki
Muktasari:
- Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imesema kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo itafanya operesheni ya kutokomeza mifuko ya plastiki nchini.
Dodoma. Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imesema kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo itafanya operesheni ya kutokomeza mifuko ya plastiki nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 26, 2022 jijini hapa kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Seleman Jafo amesema hivi karibuni watu wasio waaminifu wamegeuza vifungashio kuwa vibebeo vya bidhaa.
Amesema kutokana na hali hiyo Jumatatu ya wiki ijayo wataanza operesheni hiyo lengo likiwa ni kuyaweka mazingira katika hali ya usafi.
Waziri Jafo amesema hayo ni matakwa sheria ya mazingira sura namba 191 ya mwaka 2004 na kanuni ya 6 ya mwaka 2019 iliyopiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.
“Makamu wa Rais ameelekeza kufanyika operesheni kabambe ya kuhakikisha hakutaonekana tena mifuko ya plastiki katika mitaa yetu,”amesema Waziri Jafo.
Imeandikwa na
Lewis Mujemula na Victoria Aloyce