Serikali yatenga Sh599.7 bilioni matengenezo ya barabara

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof Makame Mnyaa Mbarawa akisoma bajeti ya Wizara yake pamoja na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2023/24 leo Jumatatu Mei 22, 2023 bungeni jijini Dodoma. Picha Merciful Munuo

What you need to know:

  • Sh599.756 bilioni zimetengwa katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya barabara kuu, barabara za mikoa, vivuko, upembuzi yakinifu wa miradi mbalimbali ya barabara.

Dar es Salaam. Ili kuhakikisha barabara kuu na zile za mikoa zinapitika vipindi vyote vya mwaka, Sh599.756 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matengenezo na ukarabati katika mwaka wa fedha 2023/2024.

 Fedha hizo za mfumo wa barabara, Sh534.66 bilioni zimeelekezwa kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Sh59.406 bilioni zikipelekwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi).

Hiyo ni kwa mujibu wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iliyosomwa leo bungeni jijini Dodoma na Profesa Makame Mbarawa ambaye anaongoza wizara hiyo.

Akisoma bajeti hiyo, Profesa Mbarawa amesema fedha zilizoelekezwa wizarani ni kwa ajili ya ukarabati wa barabara za mikoa, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara, ukarabati na ununuzi wa vivuko, usalama barabarani pamoja na usimamizi na ufuatiliaji wa miradi hiyo.

“Sh8.124 bilioni zitatumika kugharamia uendeshaji wa Bodi ya Mfuko wa Barabara,” amesema Mbarawa.

Akitoa mchanganuo wa Sh59.406 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya wizara alisema Sh15.820 bilioni ni kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara za urefu wa Km7,177.91.

Sh30.731 bilioni zimetengwa kwa ajili ya miradi ya barabara za mikoa itakayohusisha ukarabati wa jumla ya kilometa 399.23 kwa kiwango cha changarawe, ujenzi wa Km44.49 kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi na ukarabati wa madaraja/makalavati 44 katika mikoa mbalimbali nchini.

“Sh4.467 bilioni ni kwa ajili ya manunuzi na ukarabati wa vivuko pamoja na ujenzi wa maegesho na miundombinu ya vivuko, Sh3.920 nilioni ni kwa ajili ya miradi ya usalama barabarani na Mazingira,” amesema Profesa Mbarawa.

Pia ameeleza kuwa kiasi cha Sh4.467 bilioni kimeelekezwa katika usimamizi na ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa na Wizara (Ujenzi) pamoja na kujenga uwezo wa watumishi.

“Kwa upande wa jumla ya Sh534.662 bilioni za Mfuko wa Barabara ambazo zimetengwa kwa ajili ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) zitatumika kufanya matengenezo ya barabara kuu, barabara za mikoa, madaraja na uendeshaji wa mizani,” amesema Profesa Mbarawa.