Prof Mkumbo abainisha mwingiliano wa majukumu Wizara ya Elimu, Tamisemi
Muktasari:
- Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeishauri Serikali kufanya tathimini ya kina ya changamoto ya mwingiliano wa majukumu kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imesema kuna changamoto ya mgongano na mwiingiliano wa majukumu katika uendeshaji wa elimu na uendeshaji wa shule kwa upande wa elimu ya awali, msingi na sekondari.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Mei 16, 2023 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2023/24.
Amesema kuna mwingiliano wa majukumu katika uendeshaji wa elimu na uendeshaji wa shule kwa upande wa elimu ya awali, msingi na sekondari baina ya Ofisi ya Rais, Tawala la Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
“Mgongano na muingiliano unajidhihirisha katika maeneo ya utawala wa elimu, ujenzi wa miundombinu na utoaji wa miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa elimu,”amesema.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ifanye tathimini ya kina kuhusu utekelezwaji wa sera ya ugatuaji katika sekta ya elimu ili kubaini changamoto na mafanikio yake.
Aidha, Profesa Mkumbo amesema kwa kibali cha Spika wa Bunge, Kamati yake na ile ya Tamisemi zimpanga kufanya kikao cha pamoja kwa ajili ya kutafakari suala hili na kutoa ushauri wa pamoja.