Serikali yatoa mbegu za ngano bure kuwainua wakulima Makete
Mkuu wa wilaya ya Makete, Juma Sweda akimsaidia mmoja kati ya watu waliokuwa wakishusha mbegu za Ngano huko Wilayani Makete mkoani Njombe
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya, Juma Sweda, asema mbegu tani 240 zimesambazwa.
Njombe. Serikali imesema imedhamiria kuwainua wakulima wa ngano wilayani Makete kwa kuhakikisha wanaendelea kupewa mbegu bure ili wazalishe kwa wingi na kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo, Januari 21, 2025, na Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Sweda, wakati akipokea mbegu za ngano tani 240 za ruzuku zilizotolewa kwa ajili ya wakulima wilayani humo.
Amesema Serikali imedhamiria kuliinua zao la ngano na kuinua mkulima mmoja mmoja, lengo likiwa ni kupunguza kiwango cha ununuaji wa ngano kutoka nje na kuingiza hapa nchini.
Amesema wilaya hiyo ni moja wapo ya maeneo ambayo hali yake ya hewa inakubali zao la ngano katika mikoa iliyopo nyanda za juu kusini, hivyo wakulima waanze kuandaa mashamba kwa kuwa mbegu tayari zimefika.
"Ni lazima sasa usambazaji wa mbegu hizi kwenda kwa wakulima uanze, tusichelewe maana msimu wetu ni mdogo," amesema Sweda.
Ameishukuru Serikali kwa kutoa mbegu hizo kwa wananchi wa Wilaya ya Makete ikiwa ni jitihada za kuinua kilimo cha ngano nchini.
Mratibu wa zao la ngano Wilaya ya Makete, Ahmed Kichombaki, amesema wametenga sehemu tatu za upokeaji na ugawaji wa mbegu hizo za ruzuku, kuwa ni eneo la soko la ngano lililopo Kata ya Iwawa, Tandala pamoja na Mfumbi, kulingana na uhitaji wa wakulima.
Amesema mbegu hizo zimekuwa zikiuzwa Sh4,000 kwa kilo, hivyo mkulima kama angetaka kuwekeza katika kilimo hicho angelazimika kutumia Sh280,000 kwa kila ekari ili apate mbegu hizo kulingana na uhitaji.
“Lengo ni kupokea tani zaidi ya 1,000 za mbegu hii, kutokana na mahitaji makubwa ya wakulima, kuwepo kwa mashamba ya kutosha pamoja na mwamko mkubwa wa uhitaji wa mbegu za ngano,” amesema Kichombaki.
Mmoja wa wakulima wa zao la ngano Wilaya ya Makete, Jeita Mahenge, amesema soko la zao hilo limekuwa kubwa kutokana na kampuni kubwa kuingia moja kwa moja kwa wakulima kununua zao hilo.
"Zao hili linatusaidia. Tunauza na kupata hela, lakini tunatumia kuzalisha baadhi ya vyakula kama vile mikate pamoja na unga," amesema Mahenge.