Serikali yatoa Sh2 bilioni kukamilisha mradi wa maji Miwaleni
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai akizungumza na wananchi wa Miwaleni Kata ya Kahe Mashariki, Wilaya ya Moshi wakati alipotembelea mradi wa maji wa Miwaleni.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Katika kukabiliana na uhaba wa maji katika eneo la Njia panda, Mji mdogo wa Himo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro Serikali imetoa zaidi ya Sh2 bilioni kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji wa Miwaleni ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 13,000.
Moshi. Katika kukabiliana na uhaba wa maji katika eneo la Njia panda, Mji mdogo wa Himo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro Serikali imetoa zaidi ya Sh2 bilioni kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji wa Miwaleni ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 13,000.
Akizungumza na wananchi wanaozunguka eneo uliopo mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaiga amesema kukamilika kwa mradi huo kutamaliza kabisa changamoto ya maji ya muda mrefu uliopo katika eneo la Njia Panda na maeneo jirani.
"Azma ya serikali ni kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa katika ilani ya chama cha Mapinduzi, kuona maji yanafika kwenye maeneo ya wananchi,najua eneo la Njia panda mlikuwa na changamoto kubwa ya maji lakini muda sio mrefu changamoto hii inaondoka,"
"Hii ni faraja kubwa kwa wananchi wetu na naomba muwe walinzi kwenye hili eneo ambalo linazalisha maji,msipokuwa walinzi haya maji yatakauka,ni muhimu sana mlinde hili eneo lisije likavamiwa na watu ambao hawathamini mazingira kama haya,"amesema Kagaigai
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingirza Mjini Moshi(Muwsa), Kija Limbe amesema mradi huo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 50 ambapo wananchi wa Njia panda watanufaika na mradi huo.
Amesema mradi huo wa maji wa Miwaleni utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita 30 kwa sekunde ambapo ni sawa na mita za ujazo 2500 kwa siku wakati mahitaji ya maji katika eneo la Njia panda ni mita za ujazo 1190.
"Mradi huu wa maji wa Miwaleni utagharimu Sh2bilioni na utaondoa changamoto ya maji kwa wananchi wa Njia Panda na mradi huu utazalisha maji lita 30 kwa sekunde ambapo ni sawa na mita za ujazo 2500 kwa siku wakati mahitaji kwa sasa ni mita za ujazo 1190 ambapo zaidi ya wananchi 13,000 watanufaika na mradi huu,"alisema kija
Baadhi ya wananchi wa Njia Panda wakaishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo wa maji na kusema itakuwa ni suluhisho la muda mrefu kwani wamekuwa wakitaabika usiku na mchana wakigombania maji ya visima.