Serikali yatoa Sh42.3 bilioni kulipa fidia kwa wananchi Arusha

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Moshono, wakiwemo wanaotoka Mtaa wa Losirwai, katika kata hiyo wakifuatilia mkutano huo leo Ijumaa Mei 23, 2025, jijini Arusha.
Muktasari:
- Fidia hizo zimetolewa kwa mwaka huu mmoja, kati ya hizo Sh2.27 bilioni zimetolewa kwa wananchi wa Mtaa wa Losirwai, Kata ya Moshono jijini Arusha ambao wamepisha eneo kwa ajili ya matumizi ya Jeshi (977KJ).
Arusha. Wananchi 117 wa Mtaa wa Losirwai uliopo Kata ya Moshono jijini Arusha watalipwa fidia ya Sh2.27 bilioni walizokuwa wakidai baada ya kupisha eneo la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha 977 KJ.
Wananchi hao na wengine wa Kata ya Mlangarini (Arumeru), ambao bado hawajapewa fidia hiyo katika awamu hii, walikuwa wakilalamikia fidia hiyo kwa muda mrefu.
Akizungumza na wananchi hao leo Ijumaa, Mei 23, 2025, katika mkutano wa hadhara, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema fidia hiyo ni sehemu ya fidia ya Sh42.2 bilioni zilizotolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja mkoani Arusha.
Amesema kutokana na kilio cha muda mrefu cha wananchi hao, Serikali imesikia kilio chao na kuanza kulipa fidia hizo kwa awamu, ambapo kwa sasa wameanza na hao wa Moshono.
Amesema wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024, alipata taarifa kuwa mgogoro wa fidia umepamba moto na wananchi walitaka kuandamana na kufunga barabara.
“Kwenye haki hakuna chama na kwenye mkoa huu mtu anayedai haki yake, kama ana haki, tuna wajibu wa kuhakikisha analipwa haki yake. Leo nakuja nikiwa na furaha, niwashukuru kwa uvumilivu wenu. Ni miaka mingi imepita na leo kilio chenu kimesikika.
“Leo nina furaha kuwaambia wananchi 117 wa eneo la Losirwai, fedha za fidia kwa ajili yenu zimetolewa na Serikali. Ila natambua maeneo mengine kama Arumeru (Mlangarini) bado hawajapata kwenye awamu hii, ila mtapata fidia yenu,” amesema.
Akitoa takwimu za fidia za mkoa mzima, Makonda amesema kati ya fedha hizo Sh42.3 bilioni zilizotolewa katika kipindi hicho, fidia ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Karatu ni Sh5.9 bilioni, mradi wa magadi soda Engaruka Sh14 bilioni zimetolewa kama fidia kwa wananchi.
Amesema wilayani Arumeru, Sh7.9 bilioni zimelipwa kama fidia kwa ajili ya eneo la Duluti, na Sh591.64 milioni zimetolewa kwa ajili ya wananchi waliopisha barabara ya Mirongoine–Olmoti.
“Naelewa kuna maeneo mawili, matatu tunayafanyia kazi, ikiwemo Arumeru na Monduli kule, Mkoa wa Arusha tuna mpango wa ulipaji mapema wa fidia,” amesema.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Moshono, wakiwemo wanaotoka Mtaa wa Losirwai, katika kata hiyo wakifuatilia mkutano huo leo Ijumaa Mei 23, 2025, jijini Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Emanuel Masamaki ameishukuru Serikali kwa kuwalipa fidia, akisema kilio chao cha muda mrefu sasa kimesikika.
“Tunashukuru, tumeona matumaini kwani hili ni suala la muda mrefu sana. Na ukweli ni kwamba hadhara hii unayoiona hapa ilikwazika na suala hili, lakini kwa siku ya leo tunashukuru kwa hatua hii ya fidia kulipwa,” amesema.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amiri Mkalipa, amesema suala hilo lilikuwa gumu na limechukua muda mrefu.
“Mfupa huu umewashinda wengi, ila tunashukuru umeweza kutatuliwa. Ni kweli hili suala lilikuwa linatupa presha wakati wote. Umetusumbua sana kwani ni suala la muda mrefu, leo tumeanza kutua taratibu,” amesema.